WAKALA wa Nishati Vijijini (REA) imetoa sh milioni 38.2 ili kufungwa kwa mfumo wa nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dk. Samia Suluhu Hassan mkoani Ruvuma ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Shule hiyo ya kisasa yenye wanafunzi zaidi ya 540 kwa sasa ipo katika Wilaya ya Namtumbo katika Mkoa wa Ruvuma ilizinduliwa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan Septemba 27.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa shule hiyo, Mkurugenzi wa wa Mipango na Utafiti REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje amemshukuru Rais kwa kuendelea kutoa fedha zinazowezesha wakala kutekeleza miradi yake mbalimbali kwa wakati ikiwamo miradi ya nishati safi ya kupikia.
“REA tunaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali pamoja na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo na katika shule hii tumetoa sh milioni 38.2 kwa ajili ya kufungwa mifumo ya nishati safi ya kupikia tofauti na hapo awali ambapo walikuwa wanatumia kuni kupikia,” amesema Mhandisi Chibulunje.
Mhandisi Chibulunje amesema, REA itahakikisha shule mbalimbali zinafungwa mfumo wa nishati safi wa kupikia na kuachana na matumizi ya kuni na kuongeza kuwa wakala huo umesaini mikataba ya zaidi ya Sh bilioni 50 kuhakikisha taasisi zinazolisha watu zaidi ya 300 kama magereza na kambi za jeshi zinafungiwa mifumo ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma kutoka REA, Martha Chassama amesema wakala umejipanga kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia huku akiendelea kuhamasisha wananchi kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia
“Mhe. Rais amekuwa ni kinara katika kuhakikisha anaokoa Watanzania waliokuwa wanafariki au kupata madhara ya kiafya kutokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia. Na sisi kama REA tutaendelea kuhakikisha tunatoa elimu kwa umma ili lengo la kuhakikisha kufikia 2034 asilimia 80 au zaidi ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia,” amefafanua Chassama.
Awali akizungumza mara baada ya kuanza kutumia mfumo huo wa nishati safi ya kupikia, mpishi wa shule hiyo, Said Ruanda amesema kuwa awali wakati wanatumia kuni walikuwa wanatumia muda mwingi kuandaa chakula cha wanafunzi lakini pia jiko lilikuwa na moshi na joto sana.
“Kwa kweli kuna utofauti mkubwa sana toka tumeanza kupikia kwa kutumia gesi. Jikoni hamna moshi sana kama tulivyokuwa tunapikia kwa kuni lakini pia unaweza kupika ukiwa na nguo zako ulizokuja nazo na usichafuke tofauti na hapo zamani ilikuwa lazima ubadilishe nguo uvae nguo nyingine ili nguo zako ulizokuja nazo zisichafuke,” amefafanua mzee Ruanda.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.