HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imetumia kiasi cha shilingi milioni 400 kujenga hosteli tano katika shule za sekondari ili kuwapunguzia kero wanafunzi wa kike.
Afisa Mipango wa Halimashauri hiyo Athumani Nyange amesema kila hosteli imegharimu shilingi milioni 80 na kwamba fedha zilizotumka kutekeleza mradi huo zimetolewa na serikali kwa ajili ya kujenga hosteli katika shule za sekondari Matimira, Kilagano,Maposeni,Mpitimbi na Mhalule
Nyange amesema Halmashauri ilipokea fedha hizo Agosti 2020 kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 na kwamba hivi sasa kinachosubiriwa ni kuweka vitanda na hosteli kuanza kutumika rasmi.
“Kila hosteli ina uwezo wa kubeba wanafunzi 80,kila hosteli ina vyumba 20,kila chumba kinachukua wanafunzi wanne kwa niaba ya wananchi tunaishukuru sana serikali kwa sababu hosteli hizi ni ukombozi kwa watoto wa kike’’,alisema Nyange.
Selestin Mlelwa ni Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari Mhalule amesema mradi wa hosteli katika shule hiyo umekamilika na kusisitiza kuwa hosteli hiyo itakuwa ukombozi kwa watoto wa kike ambao wamekuwa wanatembea kilometa tisa kila siku kwenda na kurudi shuleni.
Patrick Matembo ni Mkuu wa shule ya sekondari Mpitimbi anaishukuru serikali kwa kuipatia shule hiyo zaidi ya shilingi milioni 106 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu ambayo ni hosteli moja imegharimu sh. milioni 80,darasa moja sh. milioni 20 na ujenzi wa choo matundu sita uliogharimu sh.milioni sita.
Elizabeth Mwakyusa ni mwanafunzi wa kidato cha sita sekondari ya Mpitimbi anatoa shukrani kwa serikali kwa kuwajengea hosteli kitendo ambacho amesema kitawaongezea wanafunzi ari ya kusoma na kuongeza ufaulu sanjari na kupunguza utoro ambao ulikuwa unachangiwa na kutembea kwa umbali mrefu kutoka kwenye makazi yao.
Halmashauri ya wilaya ya songea ina jumla ya shule za sekondari 21 kati ya hizo sekondari 16 zinamilikiwa na serikali na sekondari tano zinamilikiwa watu binafsi na Taasisi ya dini.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 7,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.