SERIKALI imetoa shilingi milioni 560.6 kutekeleza mradi wa ujenzi wa sekondari mpya ya Kungu katika Kata ya Nakayaya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa sekondari hiyo kwa sekretarieti ya Mkoa ikiongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stepehen Ndaki,Mkuu wa shule ya sekondari Kungu Ayubu Kundya amesema ujenzi huo umetekelezwa kupitia program ya uboreshaji elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Kundya amezitaja shughuli ambazo zimekamilika katika utekelezaji wa mradi huo kuwa ni ujenzi wa madarasa manane,ujenzi wa jengo la utawala, maabara,jengo la TEHAMA,maktaba,uchimbaji wa kisima na uchongaji wa barabara.
“Shule imekamilika na imechukua wanafunzi ndani ya kata za Nakayaya na Masonya ambapo kwa mwaka 2023 jumla ya wanafunzi 220 walipangiwa kuanza kidato cha kwanza katika shule hiii’’,alisema.
Hata hivyo amesema hadi kufikia Machi 31 mwaka huu wanafunzi walioripoti katika shule hiyo ni 205 ambapo amezitaja changamoto zinazosababisha mradi huo kushindwa kutekelezwa kwa asilimia 100 kuwa ni mabadiliko ya bei za viwandani,ukosefu wa bomba la kupandishia maji kwenye tanki na ukosefu wa umeme.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo,Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki ameipongeza Halmashauri ya Tunduru kwa kusimamia ipasavyo mradi huo ambao umeanza kutumika.
Hata hivyo Ndaki ameagiza changamoto zilizopo zipatiwe ufumbuzi ili mradi uweze kutoa huduma kwa asilimia 100 hivyo kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia.
Serikali kupitia program ya SEQUIP imejenga sekondari mpya tatu katika wilaya ya Tunduru ambapo kila shule imepewa shilingi milioni 470.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.