Wilaya za Namtumbo na Tunduru mkoani Ruvuma zimeingia mkataba wa biashara ya hewa ukaa (Carbon) na Kampuni ya Tanzania Carbon(CT Limited) kutoka mkoani Arusha.
Mkataba wa kuanza biashara hiyo umesainiwa kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea chini ya Usimamizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas.
Akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo,Mkurugenzi wa Kampuni ya CT Limited Marc Backer amelitaja lengo la Kampuni ya Carbon Tanzania kuwa ni kuhakikisha wananchi wanafaidika kiuchumi na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kupanda miti.
Amesema hapa nchini wananchi wa vijiji nane katika Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi wameingiza zaidi ya bilioni 2.3 kwa kufanya biashara ya hewa ya ukaa.
“Mradi huu umewanufaisha wananchi wa wilaya za Tanganyika mkoani Katavi na Kiteto mkoani Manyara,hapa Ruvuma mradi wa biashara ya kaboni utakuwa mkubwa sana,tumeshapima tumegundua kuna kaboni nyingi sana’’,alisisitiza Backer.
Backer amesema biashara ya hewa ya ukaa ilianza rasmi mwaka 2018 katika Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi kwa kuendeshwa na Taasisi ya Carbon Tanzania ambapo mapato ya biashara hiyo yamekuwa yakipanda mwaka hadi mwaka.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Wakili Julius Mtatiro ameitaja mikataba ya biashara ya kaboni kuwa ina faida kubwa hata kama msitu utatunzwa kwa miaka 60 unaleta faida kwa wananchi wenye misitu ikiwa ni Pamoja na kuleta mvua nyingi na kwamba wananchi watapata fedha nyingi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Ngollo Malenya amesema biashara ya hewa ukaa ni mradi mpya hapa nchini na kwamba baada ya majaribio katika wilaya ya Tanganyika serikali imeona faida kubwa.
Amesema biashara hiyo inamwezesha mwananchi kupata fedha baada ya kupanda miti ambapo ameitaja wilaya ya Namtumbo kuwa ni wilaya ya kimkakati kwa kuwa asilimia 19 ya maji yanayoingia kwenye mradi wa bwawa la Mwalimu Nyerere Rufiji yanatoka Namtumbo.
Amesisitiza kuwa biashara ya hewa ukaa ni mradi ambao utasaidia kutunza mazingira na kuhakikisha kuwa uharibifu wa mazingira unakwisha na kwamba mradi utaleta mvua za kutosha na dhana ya Mkoa wa Ruvuma kuwa ghala la Taifa la chakula itaendelea kuwepo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki amewaasa wakulima kuhakikisha wananufaika na mradi wa kaboni kwa kuhakikisha wanapanda miti ya kutosha badala ya kuishia kulima mahindi na mazao mengine.
Amewaasa wakulima kupanda miti kwa wingi na kuhifadhi misitu ili kupunguza hewa ya ukaa na kuongeza upatikanaji wa hewa safi lakini pia watakuwa wanafanya biashara ya hewa ya ukaa.
Tanzania imesaini mikataba ya Kimataifa ambayo inahamasisha biashara ya hewa ya ukaa Duniani ambapo wananchi wanapopanda miti na kuhifadhi misitu inasaidia kufyonza na kupunguza hewa ya ukaa hewani na kulipwa fedha hivyo kukuza uchumi wao.
Soko la hewa Safi ya Kaboni lililopo ni fursa muhimu kwani Dunia imedhamiria kuboresha Anga kutokana na madhara ya uharibifu wa hewa chafu ya kabon ili kuokoa anga na ongezeko la Joto duniani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.