MKOA WA RUVUMA UNA ZIADA YA CHAKULA ZAIDI YA TANI LAKI SABA
Mkoa wa Ruvuma una kiwango cha utoshelevu wa chakula kwa zaidi ya miaka 12 mfululizo.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameyataja mahitaji ya chakula mkoani Ruvuma kwa msimu wa mwaka 2022/2023 ni tani 469,172 na kuufanya Mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 787,190.
Hata hivyo amesema chakula ambacho kilizalishwa katika msimu wa mwaka 2021/2022 kinatumika katika msimu huu wa mwaka 2022/2023 ambapo katika mazao ya chakula zilizalishwa tani 1,256,362.
“Mkoa wa Ruvuma ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula na biashara,kwa miaka minne mfululizo mkoa umeendelea kupu la chakula la Taifa kwa kuongoza kitaifa katika uzalishaji wa chakula nchini’’,alisema RC Thomas.
Akizungumzia mazao ya biashara,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameyataja mazao ya kimkakati yanayowaingizia wakulima kipato kuwa ni zao la kahawa ambapo katika msimu wa mwaka 2021/2022 jumla ya kilo milioni 13.7 ziliuzwa na kuingiza jumla ya shilingi bilioni 97.
Mazao mengine ya kimkakati ameyataja kuwa ni zao la ufuta ambalo katika msimu uliopita limewaingizia wakulima shilingi bilioni 23.4,zao la soya limeingiza bilioni sita na zao la mbaazi limeingiza shilingi bilioni 1.3.
Amesema katika msimu ujao wa kilimo Mkoa wa Ruvuma unahitaji mbolea tani 50,280 ambapo hivi sasa usajili wa wakulima kwa ajili ya mbolea ya ruzuku unaendelea na hadi sasa wakulima 216,366 wamejasiliwa kwenye vitabu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Septemba 12,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.