Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema hadi kufikia Mei 26 mwaka huu katika vituo vyote nane vya kulaza wagonjwa wa corona hakuna mgonjwa hata mmoja.
Mndeme ametoa taarifa hiyo leo, wakati anapokea msaada wa vifaa vya kujikinga na corona kutoka Kampuni ya Mafuta ya Refueling Solutions ambayo imetoa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 10.9.
Amesema vifaa hivyo vitakwenda kutumika katika harakati za mapambano dhidi ya corona kwa sababu ugonjwa huo bado upo nchini na mapambano yanaendelea hadi ugonjwa huo utakatokomezwa kabisa.
“Naomba mtufikishie salama zetu kwa uongozi mzima wa Refueling Solutions,tangu tumeanza kupokea misaada ya vifaa vya kukabiliana na corona hatujawahi kupata msaada mkubwa kama huu tunashukuru sana’’,alisema.
Amesema kitendo cha kutoa msaada huo kimedhihirisha uzalendo wa hali ya juu katika kuunga mkono juhudi za Rais Dkt.John Magufuli kwenye mapambano ya corona.
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa hivyo,Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Refueling Solutions Ahamad Sweya amevitaja vifaa vilivyotolewa na Kampuni hiyo kuwa ni barokoa boksi 35, vipima joto la mwili (thermal scanner)13,mipira ya kuvaa mikononi (gloves) boksi 15 na mavazi meupe ya watoa huduma 100.
Virusi vya corona ni janga la Dunia kwa kuwa hadi sasa inakadiriwa duniani kote watu zaidi ya milioni tano wameambukizwa corona kati yao watu zaidi ya milioni mbili wamepona na vifo ni zaidi ya laki tatu.
IMEANDIKWA NA ALBANO MIDELO
AFISA HABARI MKOA WA RUVUMA
MEI 26,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.