MKOA wa Ruvuma, umeweka lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la korosho ghafi kutoka tani 25,284 katika msimu wa kilimo wa 2021/2022 hadi kufikia tani 700,000 ifikapo mwaka 2025/2026.
Mkuu wa mkoa huo Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge alisema hayo jana, wakati akifungua kikao kazi cha kutambulisha mpango wa uboreshaji wa usimamizi wa huduma za ugani kwa wakulima wa zao la korosho kilichofanyika wilayani Tunduru.
Alisema, kwa sasa mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache hapa nchini inayozalisha korosho kwa wingi,ambapo unashika nafasi ya tatu kitaifa ukiongozwa na mikoa ya Lindi na Mtwara,hata hivyo lengo la mkoa ni kuongeza uzalisha kuanzia msimu 2022/2023 ili kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.
Ibuge alisema,ongezeko la uzalishaji wa zao hilo kutachangiwa na usimamizi na utoaji wa huduma bora za ugani kipindi cha uzalishaji ambapo Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na wadau wengine imejipanga kuhakikisha mkulima anapewa mbinu bora za kuhudumia mikorosho.
Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kwa uamuzi wa kutoa pembejeo za korosho kwa wakulima bure,hali iliyowezesha wakulima wengi kuongeza ukubwa na wengine kufufua mashamba ya zamani, jambo lililosaidia kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 24,000 mwaka 2020 hadi tani 25,284,493 mwaka 2021.
Amewapongeza wakulima wa zao hilo na wadau wa sekta ya kilimo kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika msimu wa kilimo 2021/2022 ambapo mkoa huo umevuka lengo la uzalishaji.
Hata hivyo,amewahimiza wakulima na watendaji wenye dhamana ya kusimamia kilimo cha korosho kuhakikisha korosho zinazoendelea kulimwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo zinakuwa na ubora na tamu ili kuwa na soko la uhakika ndani na nje ya nchi yetu.
Alisema, takwimu za uzalishaji wa zao la korosho katika mkoa huo zinaonesha kuongezeka mwaka hadi mwaka katika kipindi cha miaka minne mfululizp kutoka msimu wa kilimo 2017/2018 hadi msimu wa 2021/2022 ambapo kilo 104,819,739 za korosho zilikusanywa na kuuzwa kwa bei ya Sh.2,802.
Aidha alieleza kuwa,katika msimu wa 2021/2022 pekee mkoa huo ulifanikiwa kuzalisha na kukusanya jumla ya kilo 25,284,493 zenye thamani ya Sh.bilioni 50,610,456,426 ambazo ziliuzwa kwa bei ya Sh.1,971.60 kwa kilo.
Alisema,ongezeko la uzalisha limetokana mara baada ya kuanzisha na kuendelea kusimamia kikamilifu mfumo wa stakabadhi ghala ambao umewezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei kubwa ya Sh.2,802 kwa kilo ikilinganishwa na bei kabla ya mfumo huo ambayo ilikuwa Sh.700 hadi 800.
Alisema,katika kuendeleza zao la korosho juhudi nyingi zimefanywa na kutekelezwa na wadau mbalimbali ikiwamo Serikali ambayo katika msimu wa mwaka 2021/2022 ilisambaza kilo 7,183 za mbegu,kilo 1,569,525 za viuatilifu vya Salfa ya unga na viuatilifu vya maji lita 89,717,kusajili wakulima wa korosho 37,000 na kutoa mafunzo kwa maafisa ugani.
Alisema,zao la korosho ni moja ya mazao makuu wa kilimo katika mkoa huo ambalo lina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa Mkoa,Taifa na mkulima mmoja mmoja ambapo kwa sasa wakulima wengi wameweza kuboresha maisha yao na kujitegemea kupitia kilimo cha zao hilo.
Jenerali Ibuge alisema,uzalishaji wa zao la korosho umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na wadau wote kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya zao hilo,zikiwamo huduma za ugani.
Kwa mujibu wake, licha ya mkoa huo kuongoza kwa uzalishaji mkubwa wa chakula kwa miaka minne mfululizo hapa nchini,lakini kilimo chake hakina tija kubwa kutokana na wakulima kutumia jembe la mkono badala ya zana za kisasa.
Amewataka maafisa ugani na wataalam wengine wa kilimo kuacha tabia ya kukaa ofisini, badala yake kwenda kuwatembelea wakulima mashambani ili kuwapa elimu kuhusu kilimo bora na chenye tija.
Katibu Tawala wa mkoa huo Stephen Ndaki alisema, wakulima wa mkoa wa Ruvuma bado wana uhitaji mkubwa wa teknolojia ya kisasa katika shughuli zao za kilimo na sio vinginevyo.
Alisema,mkoa huo kupitia Halmashauri zote nane zina uwezo wa kulima zao la korosho kunatokana na kuwepo kwa hali nzuri ya hewa na ardhi inayofaa kwa korosho badala ya kulimwa katika Halmashauri mbili tu za Tunduru na Namtumbo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania Francis Alfred alisema,katika utekelezaji wa mpango huo Bodi ya korosho itashirikiana na sekretalieti za mikoa na Mamlaka za serikali za mitaa ili kuhakikisha huduma za ugani zinawafikia wakulima.
Alisema,bodi itatoa motisha kwa wataalam watakaotekeleza mpango huo kwa ufanisi mkubwa katika maeneo yao ambapo itatenga jumla ya Sh.milioni 200 kwa ajii ya uhamasishaji huo ambao utakwenda sambamba na utoaji elimu ya kilimo bora cha zao la korosho kwa vitendo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.