Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma Emmanuel Kisongo amewataka wazabuni wanaosambaza vyakula katika shule za bweni kuleta chakula kilicho bora ili kusaidia kuondoa udumavu.
Kisongo amesema hayo wakati anazungumza katika kikao kazi cha kuboresha afua za afya na lishe katika shule za bweni Mkoa wa Ruvuma ambacho kilihudhuriwa na wadau mbalimbali na kufanyika katika ukumbi wa sekondari ya Songea Girls.
Afisa Elimu huyo amesema kufanyika kwa kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa viashiria vya mkataba walishe unaozitaka shule zote kutumia vyakula vyenye viinilishe kwa wingi ili kuboresha lishe kwa vijana wa rika balehe.
“Tunatakiwa kupeana mbinu mbadala za kupata vyakula ambavyo vitasaidia kupunguza tatizo la udumavu, pia tunahimizwa matumizi ya vyakula vyenye virutubishi kama viazi lishe na mahindi lishe ulimaji wa bustani za mboga na matunda sambamba na matumizi ya mazao ya bustani’’,alisisitiza Kisongo.
Kwa upande wake Afisa Lishe Mkoa wa Ruvuma Neema Mtekwa amesema ni muhimu sana kuwekeza katika lishe hasa hizo siku 1000 za uhai wa mtoto, na kwamba kuna visababishi vya utapiamlo ambavyo ni ulishaji hafifu kwa watoto, vijana na makundi mengine maalumu.
Kulingana na Afisa Lishe huyo, utafiti ulifanyika hivi karibuni umebaini kuwa angalau watoto wanaopewa chakula chenye mchanganyiko unao hitajika ni asilimia 20.6.
Naye,Mwakilishi wa Afisa Ununuzi Mkoa wa Ruvuma Anthony Luoga, amewaomba wazabuni wajitahidi kuleta chakula chenye ubora ili kusaidia kupunguza udumavu kwa watoto ambao wanaishi katika shule za bweni.
Mwezeshaji kwenye kikao hicho David Mwasanga amewasisitiza elimu ya kilimo cha mahindi na mbogamboga kwa wadau ili kuboresha lishe na kuondokana na udumavu kwa watoto.
Kikao kazi hicho kilishirikisha wataalam wa lishe,elimu,ununuzi,kilimo ,wazabuni,walimu wa chakula na wakuu wa shule za bweni
Imeandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Farida Mussa Baruti
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.