MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kutoa chanjo mbalimbali ikiwemo chanjo kwa Watoto chini ya miaka mitano kwa asilimia zaidi ya 100 hadi kufikia Juni 2023.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amezitaja chanjo hizo ambazo zinatolewa bure kwa akinamama na Watoto wenye umri chini ya miaka mitano kuwa ni chanjo ya kuzuia kifua kikuu (BCG) ambayo imetolewa kwa asilimia 143 na chanjo ya kuzuia polio (OPV3) ambayo imetolewa kwa asilimia 125.
Amezitaja chanjo nyingine kuwa ni chanjo ya surua imetolewa kwa asilimia 122.5,kuzuia kuharisha kwa asilimia 103,pepopunda kwa akinama kwa asilimia 103 na chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 imetolewa kwa asilimia 115.5
“Katika kuhakikisha hali ya lishe inapata kipaumbele kwa Watoto chini ya miaka mitano,Mkoa na wadau mbalimbali wameendelea kufuatilia hali ya lishe na kutoa ushauri kwa Watoto ambao wanaonekana kuwa na matatizo mbalimbali ya afya na wale ambao wanahitaji matibabu hutibiwa bure’’,alisisitiza.
Hata hivyo Kanali Thomas amesema bado hali ya lishe kwa Watoto walio chini ya miaka mitano hairidhishi licha ya Mkoa wa Ruvuma kuwa gwiji la chakula nchini.
Ametoa rai kwa wazazi na walezi kuzingatia malezi na lishe kulingana na maelekezo ya watalaam wa afya ikiwemo Watoto kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi sita ya mwanzo,Watoto kupewa vyakula safi na vyenye mchanganyiko wa viinilishe.
Naye Mratibu wa Lishe Mkoa wa Ruvuma Neema Mtekwa amewashauri wazazi na walezi kuhakikisha Watoto wao wanapewa nyongeza ya vitamini A ili kuwakinga na maradhi,upofu,surua na kuboresha afya ya Ngozi.
Mtekwa ameshauri Watoto wapimwe hali zao za lishe ili kujua kama wamedumaa,wana uzito pungufu na ukondefu ili wapatiwe viinilishe.
Utafiti wa mwaka 2022 unaonesha kuwa asilimia ya Watoto waliopata udumavu mkoani Ruvuma ni asilimia 35.5 ukilinganisha hali ya udumavu kitaifa ambayo ni asilimia 30.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.