Na Albano Midelo
MKOA wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache maarufu nchini inayozalisha chakula na kutoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.
Hayo yamesema na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati wa kufunga maonesho na sherehe za wakulima Nanenane ngazi ya Mkoa wa Ruvuma zilizofanyika katika viwanja vya Amanimakoro wilayani Mbinga.
Amesema chakula kinachozalishwa mkoani Ruvuma licha ya kutumika ndani ya Mkoa ,lakini pia kinatumika nje ya Mkoa na nje ya nchi hivyo kusaidia wananchi kupata kipato na kukuza uchumi.
Hata hivyo amewatahadharisha wananchi kutouza chakula chote badala yake wakumbuke kuweka akiba ya chakula ambacho kitawafikisha katika msimu mwingine wa mavuno.
“Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoka Bilioni 275 hadi bilioni 295 mwaka huu,imeongeza pia bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Zaidi ya shilingi bilioni 294 hadi kufikia shilingi Trilioni 1.3,hii yote ni dhamira thabiti ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuinua sekta ya Kilimo,Uvuvi na Mifugo’’,alisema Kanali Abbas.
Katika hatua nyingine,Mkuu wa Mkoa ametoa maagizo mbalimbali kwa watendaji wa Halmashauri na Wilaya yakiwemo kusimamia matumizi sahihi ya vitendeakazi vilivyotolewa na serikali kwa maafisa Ugani,kuhakikisha uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unafanyika kwa utulivu na amani na kuhakikisha shule zenye maeneo yanayofaa wapande maharage lishe na miti ya matunda ili kusaidia wanafunzi kupata lishe.
Maagizo mengine ni Kamati za Pembejeo ngazi ya Wilaya zihakikishe zinakuwa na vituo vya kusambazia mbolea za ruzuku ya serikali na wataalam wa ufugaji Samaki waendelee kutoa elimu ya utengenezaji chakula cha Samaki na kuandaa mazingira wezeshi ya uwekezaji vyakula vya samaki.
Awali akizungumza kwenye maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mheshimiwa Kisare Makori amesema Zaidi ya asilimia 85 ya wananchi wilayani Mbinga ni wakulima wa mazao ya chakula na biashara.
Makori ameahidi kusimamia kilimo ili Wilaya hiyo iweze kutoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo na kuufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa kinara katika uzalishaji wa mazao ya chakula na wananchi waendelee kufaidika kupitia sekta ya kilimo.
Amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kulifanya eneo la Amanimakoro kuwa endelevu katika maonesho ya Nanenane ya Mkoa kila mwaka ombi ambalo Mkuu wa Mkoa ameridhia.
Kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya sherehe za wakulima Nanenane ni Chagua viongozi bora wa serikali za mitaa kwa maendeleo endelevu ya kilimo,mifugo na uvuvi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.