MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewapongeza wadau wa elimu katika Mkoa kwa kuwezesha ufaulu mzuri wa asilimia 98.68 katika matokeo ya kidato cha sita kitaifa mwaka 2020.
Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anafungua Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini Songea.
Ameyataja matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2020 katika Mkoa wa Ruvuma,yanaonesha kuwa ufaulu ulikuwa kwa asilimia 78.52 na ufaulu wa mwaka 2019 ulikuwa ni asilimia 85.70 hivyo ameagiza kuongeza jitihada za kuongeza ufaulu.
“Hata hivyo Naipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kufaulisha darasa la saba kwa asilimia 85.51.Aidha Halmashauri ya Wilaya ya Songea inatakiwa kuongeza juhudi ili kupandisha ufaulu zaidi kwani matokeo yanaonesha wamefaulisha kwa asilimia 66.68’’,alisisitiza Mndeme.
Hata hivyo Mndeme amesema miundombinu kwa ajili ya Wanafunzi wa kidato kwanza 2021,inaonesha kuwa hadi kufikia Novemba 2020 kulikuwa na upungufu wa vyumba 43 kwaajili ya kidato cha kwanza mwaka 2021.
“Nimetoa maelekezo kwa Halmashauri zote kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanaanza masomo Januari 2021,Tumejipanga vizuri hakuna mtoto atakaebaki nyumbani kwa kukosa nafasi na Mkoa wetu ni kati ya Mikoa 9 nchini ambayo wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza watapata nafasi’’,alisema.
Hata hivyo Mndeme amesema Mkoa unatekeleza Kampeni ya Magauni manne chini ya Kaulimbiu ya Niache Nisome,ambapo Serikali ya Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Elimu inapambana na kuhakikisha inaondoa vikwazo vinavyosababisha wanafunzi wa kike kushindwa kuhudhuria masomo.na kumaliza.
Amevitaja vikwazo hivyo kuwa ni Mimba za utotoni hali inayosababisha wanafunzi wakatishe masomo na kufifisha ndoto zao.
Katika kupambana na kikwazo cha mimba za utotoni,Mndeme amesema Mkoa kupitia Halmashauri zake umejenga Shule za wasichana pamoja na kujenga Hosteli kwa shule za kutwa ili kuwasaidia wanafunzi wa kike kuepuka vikwazo hivyo.
Amezitaja shule hizo kuwa zimejengwa katika Halmashauri zote za Mkoa wa Ruvuma isipokuwa Halmashauri ya Madaba ambapo Kamati ya Ushauri ya Mkoa imeona umuhimu wa kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa katika Halmashauri ya Madaba itakayo chukua wanafunzi kutoka maeneo yote ya Mkoa.
Imeandaliwa Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 14,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.