MKOA wa Ruvuma umepokea kilo Elfu 52,712 ya mbegu bora ya zao la Alizeti zenye thamani ya Sh.184,492,000 kutoka kwa wakala wa Mbegu Tanzania(ASA)ambazo zitauzwa kwa bei ya Sh.3,500 kwa kilo moja kwa wakulima wa mkoa huo katika msimu 2021/2022.
Hayo yamesemwa na Afisa Kilimo wa mkoa huo Onesmo Ngao,wakati akitoa taarifa ya kuwasili kwa mbegu hizo kwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge.
Ngao alisema, kawaida mbegu hizo uuzwa kwa bei ya Sh.35,000 kwa kilo moja na wafanyabiashara, lakini serikali imeweka punguzo hadi kufikia Sh.3,500 kama jitihada za kuwawezesha wakulima wengi waweze kununua na kulima zao hilo.Alisema,mkoa wa Ruvuma umejipanga kutekeleza kilimo cha mkataba ili kuunga mkono juhudi za Serikali ambapo umepanga kulima hekta 9,291 ambazo zinatarajia kutoa mavuno ya tani 7,743 katika msimu wa kilimo 2021/2022.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amewaomba wakulima wa mkoa huo kupitia Halmashauri za wilaya kutumia fursa hiyo kupata mbegu bora, kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Alisema, ni matumaini ya Serikali ya mkoa na Taifa kuwa, mbegu hizo zitasaidia wakulima wengi kulima zao la Alizeti na hatimaye kufikia adhima ya Serikali kuwezesha upatikanaji wa mafuta ya kula ndani na nje ya mkoa.
Aidha Ibuge, amewataka kulima kwa kufuata maelekezo ya wataalam na kuwatumia maafisa ugani waliopo katika maeneo yao, na watoa huduma za pembejeo kulima kilimo cha kisasa badala ya kuendelea kulima kwa mazoea.
Ametoa wito kwa maafisa ugani kutimiza wajibu wao,na kuwahudumia wakulima ili mbegu hizo zilete tija katika uzalishaji na kuwanufaisha wakulima ambapo mkoa umejipanga kuhakikisha wanatumia mvua zilizoanza kunyesha kulima mazao mbalimbali ya chakula na biashara.
Alisema,lengo la Serikali ni kuleta tija na kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula ndani ya mkoa na nchi kwa ujumla, na kuipunguzia serikali gharama ya kuagiza mafuta hayo nje ya nchi ndiyo maana imewekeza nguvu kubwa kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo unaongezeka.
Ibuge ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan,kumsaidia mkulima kupata mbegu hizo kwa bei ya ruzuku kupitia wakala wa mbegu Tanzania(ASA)kwa kuwa zao hilo ni la kimkakati hali itakayowezesha watu wenye kipato cha chini kumudu bei.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.