MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amezindua jengo la mahakama ya mwanzo ya Nakapanya wilayani Tunduru lililogharimu zaidi ya shilingi milioni 55.
Ujenzi wa mahakama hiyo umetokana na agizo la Rais Dkt John Magufuli wakati wa ziara yake ya Aprili 4 mwaka jana aliposimama katika tarafa ya Nakapanya kuwasalimia wananchi na kusikiliza kero zao.
Akizungumza kabla ya kuzindua jengo hilo,Mkuu wa Mkoa alisema wananchi hao walitoa kwa Rais, kero ya kufungwa kwa soko kwa sababu ya kuwa karibu na mahakama ndipo Rais Magufuli aliagiza litafutwe eneo jingine la kujenga mahakama hiyo.
“Katika kuunga mkono juhudi za ujenzi wa mahakama hii Rais alichangia shilingi milioni 10,tunamshukuru kwa moyo wake anavyojitolea kumaliza kero za wananchi wa Tanzania tukiwemo sisi wananchi wa Nakapanya’’,alisema Mndeme.
Mndeme amewaagiza TARURA kutengeneza barabara inayokwenda katika mahakama hiyo katika kiwango cha changarawe ili iweze kupitika mwaka mzima,pia amemwagiza Meneja wa TANESCO na RUWASA kupeleka umeme na maji katika jengo hilo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amebainisha gharama zilizotumika katika ujenzi huo na wadau waliochangia hadi sasa kuwa ni Rais Dkt John Magufuli shilingi milioni 10,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma shilingi milioni 29,mfuko wa Jimbo milioni tatu na nguvu za wananchi zaidi ya milioni tatu.
Amesema mradi ulianza kutekelezwa Mei 2019 na ulitarajia kugharimu zaidi ya milioni 69 hadi kukamilika na kwamba kutokana na matumizi ya force account gharama halisi za ujenzi zimepungua na kufikia zaidi ya milioni 55.
“Jengo hili lina vyumba vinne vya ofisi,ukumbi mmoja,vyumba viwili vya mahabusu,choo cha ndani na vyoo viwili vya nje,mradi utasaidia kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa mahakama’’,alisisitiza Mtatiro.
Mtatiro amesema,mradi huo utawanufaisha kwa kupata haki za kisheria wananchi wa tarafa nzima ya Nakapanya yenye kata za Nakapanya, Namakambale, Tinginya, Ngapa, Mindu, Namiungo, Majimaji na Muhuwesi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa jengo hilo,Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea Jaji Isaya Alufan amempongeza Rais kwa maamuzi ya busara kuamua kujenga mahakama ya mwanzo Nakapanya ambapo amesema mahakama ni sehemu ya kutoa huduma kwa wananchi.
Hata hivyo amesema vitu vichache ambavyo ni maji,umeme na samani vikikamilika jengo hilo litaanza kutoa huduma kwa wananchi ,ameahidi Idara ya Mahakama ipo tayari kushirikiana na serikali kuhakikisha kuwa mapungufu yanafanyiwa kazi haraka ikiwemo kuwaleta watumishi wa mahakama na samani ili kazi ianze.
Kukamilika kwa mahakama ya mwanzo Nakapanya kunaifanya wilaya ya Tunduru kuwa na mahakama za mwanzo saba.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Mei 23,2020
Tunduru
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.