MKOA wa Ruvuma umefanikiwa kutoa chanjo ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 122 .
Akizungumza kwenye kikao cha Mkoa cha utekelezaji wa kampeni ya utoaji wa huduma za chanjo ya polio kilichofanyika mjini Songea,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amesema Mkoa umepata mafanikio makubwa katika awamu ya kwanza ya utoaji chanjo ya polio.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Pololet Mgema,amesema katika awamu ya kwanza ya utoaji chanjo ya polio,Mkoa ulipanga kuchanja watoto 241,966 ambapo waliochanjwa walikuwa ni watoto 293,543 sawa na asilimia 122.
‘’Mkoa wa Ruvuma umekuwa kinara katika utoaji chanjo ya polio kati ya mikoa minne ya awamu ya kwanza iliyotekeleza kampeni,pia Mkoa wa Ruvuma ulikuwa kinara kwa utaoji chanjo za kawaida mwaka 2021’’.alisisitiza RC Ibuge.
Kwa mujibu wa RC Ibuge, katika chanjo ya UVIKO 19 ambayo Mkoa ulianza kuchanja Agosti 2022,Mkoa umechanja jumla ya watu 409,323 kati yao watu 322,363 sawa na asilimia 78.76 wamekamilisha dozi na watu 86,960 wamepata dozi ya kwanza.
Hata hivyo amesema ili kufikia asilimia 70 ya uchanjaji Mkoa wa Ruvuma,unatakiwa kuchanja watu 670,557 ambao ni asilimia 70 ya watu 957,938 wenye umri wa Zaidi ya miaka 18 ambao ndiyo wenye sifa ya kupatiwa chanjo ya UVIKO.
Amesema hadi kufikia Mei 15 mwaka huu,Mkoa wa Ruvuma umechanja watu 322,363 ambao wamekamilisha dozi sawa na asilimia 48.07 ya watu 670,557.
Kwa upande wake Mratibu wa chanjo Mkoa wa Ruvuma Winbroad Mvile amelitaja lengo la kampeni za utoaji huduma za chanjo ya polio ya matone kwa watoto chini ya miaka mitano ni kuzuia uwekezekano wa watoto kupata madhara yatokanayo na virusi vya polio.
Hadi sasa visa viwili vya polio vimegundulika katika nchi mbili jirani na Mkoa wa Ruvuma za Malawi na Msumbiji hivyo chanjo inasaidia kuzuia mlipuko wa ugonjwa huo kwa watoto baada ya kupata chanjo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Mei 19,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.