Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Jumanne Mohamed Nkana anasema soko la wazi la madini ya vito na dhahabu la mjini Songea lilifunguliwa Mei 3,2019 na soko la Tunduru lilifunguliwa Mei 27,2019.
Anasema tangu kufanyika kwa ufunguzi wa masoko hayo hadi kufikia Desemba 31, 2019,jumla ya gramu 206,712 za madini ya vito ziliuzwa sokoni zikiwa na thamani ya shilingi zaidi milioni 513.
Anautaja mrabaha uliolipwa kutokana na mauzo hayo ni zaidi ya milioni 32 na ada ya ukaguzi iliyolipwa serikalini ni milioni 5.4 na kodi ya huduma kwa Halmashauri husika ni zaidi ya milioni 1.5.
Kwa mujibu wa Mhandisi Nkana,madini ya dhahabu katika kipindi hicho zimeuzwa jumla ya gramu 24,415.96 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.310 ziliweza kuuzwa katika soko la madini la Songea.
Anautaja mrabaha ambao ulilipwa serikalini kutokana na mauzo ya dhahabu ni zaidi ya shilingi milioni 138 na ada ya ukaguzi iliyolipwa ni zaidi ya milioni 23 na kodi ya huduma iliyolipwa kwa Halmashauri husika ni zaidi ya milioni 6.9.
“Kwa ujumla katika masoko yote mawili ya Tunduru na Songea tangu kuanzishwa kwa masoko haya hadi kufikia Desemba 31,2019 madini ya vito na dhahabu yaliyouzwa yalikuwa na uzito wa gramu 231,128.2 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.824’’,anasema.
Mhandisi Nkana anautaja mrabaha wa jumla uliolipwa serikalini ambao umetokana na mauzo ya madini ya dhahabu na vito katika kipindi hicho kuwa ni zaidi ya shilingi milioni 171 na ada ya ukaguzi iliyolipwa serikalini ni zaidi ya milioni 28.5 na kodi ya huduma ya jumla iliyolipwa katika Halmashauri husika ni zaidi ya milioni 8.4.
Hata hivyo Nkana anakiri kuwa tangu kuanzishwa kwa masoko ya wazi ya madini ya vito na dhahabu kuna mafanikio kwa sababu kabla ya soko kuanzishwa kulikuwa hakuna takwimu zozote za mauzo ya madini kwa sababu wafanyabiashara wengi walikuwa hawalipi mrabaha na kodi nyingine zinazotakiwa kulipwa kwa mujibu wa sheria na mikataba ya madini.
Anasema katika kipindi cha nyuma sheria ilikuwa haijawabana kiasi cha kutosha na kwamba baada ya serikali ya Awamu ya Tano kufanya marekebisho ya sheria ya madini mwaka 2017 na kuanzisha soko la wazi la madini watu wengi hivi sasa wanafanya biashara ya madini kwa kuzingatia sheria.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.