Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob John Mkunda, amewataka wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuokoa Taifa dhidi ya maadui ujinga, maradhi na umasikini, pamoja na kuwaenzi mashujaa waliopigana na kufa kwa ajili ya Taifa.
Ametoa rai hiyo wakati akisoma hotuba kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya mashujaa wa Vita vya Majimaji, ambapo alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea
"Rai yangu ni kwamba mashujaa waliolala mahali hapa na kwingineko watutie hamasa kupambana kadri tuwezavyo ili kuokoa Taifa letu dhidi ya maadui hao, maana bado wapo. Kuendekeza uvivu, uzembe, madawa ya kulevya, rushwa, ubadhilifu wa mali za umma na malalamiko bila kufanya kazi ni kuzisaliti roho zilizoangamizwa na wakoloni kwa ajili yetu," alisema Jenerali Mkunda.
Pamoja na mambo mengine, Jenerali Mkunda amesema mashujaa hao waliangamia kuulinda utamaduni wa Mtanzania, na hivi sasa vilio ni vingi vya mmonyoko wa maadili ya kitanzania, hali inaonyesha kuwa msimamo wa mashujaa umeachwa, hivyo ni wakati wa kujitathmini na kuwaenzi mashujaa kwa kuuenzi utamaduni uliolindwa na mashujaa kwani ndio unaotambulisha Taifa la Tanzania.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema maadhimisho hayo, ambayo yamekuwa yakiratibiwa na Ofisi ya Mkoa, Wizara ya Maliasili na Utalii, na Baraza la Mila na Desturi la mkoa, licha ya kuwakumbuka mashujaa, kwa mwaka huu Wizara husika imeamua kutumia maadhimisho hayo kuhamasisha utalii wa utamaduni na malikale ili kujiletea maendeleo na kutia chachu ya maadhimisho hayo.
Kanali Ahmed ameongeza kuwa, kupitia maadhimisho hayo, Mkoa umeendelea kupata fursa za kiuchumi kupitia wageni mbalimbali waliokuja kwa ajili ya maadhimisho hayo na kutembelea vivutio vilivyopo mkoani hapo.
Kwa upande wake, Chifu wa Wangoni, Emmanuel Zulu, amesema wamekuwa wakiziheshimu sana kumbukumbu hizo na zina machungu mengi kutokana na kile walichotendewa mashujaa wa Vita vya Majimaji.
Kilele cha maadhimisho ya kumbukizi ya mashujaa wa Vita vya Majimaji hufanyika Februari 27 kila mwaka, ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni "Makumbusho ya Majimaji na Malikale Zetu kwa Maendeleo ya Utalii na Uchumi."
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.