MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amewaagiza viongozi wa wilaya ya Namtumbo kuongeza kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine ya elimu kukamilika kabla ya Tarehe 10 Mwezi Desemba mwaka huu.
Ibuge ametoa agizo hilo jana, wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa kupitia mpango wa maendeleo wa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Covid 19 wilayani humo.
Mkuu wa mkoa alisema,hajaridhishwa na na kasi ya utekelezaji wa miradi ya Covid -19 katika wilaya hiyo kwa kuwa,bado ujenzi wake unakwenda kwa kusua sua ikilinganisha na miradi inayojengwa kwenye wilaya nyingine, ambapo ametoa wiki mbili wawe wamekamilisha kazi hiyo.
“ maeneo mengine nimekuta mafundi zaidi ya mmoja katika darasa ,kuna wanaopiga lipu,kufunga milango,madirisha, na kupaua lakini katika miradi yenu hapa mafundi ni wachache,kwa hiyo naagiza miradi yote iwe imekamilike kabla ya tarehe 10 Desemba” alisema Ibuge.
Aidha amewataka viongozi wa wilaya hiyo, kuhakikisha vifaa vinavyotumika katika ujenzi huo vinakuwa na ubora unaotakiwa ili kuwezesha kupata madarasa bora na viwango vya hali ya juu badala ya kujenga kwa kubabaisha.
Ibuge,ametaka kila mmoja kusimamia miradi hiyo kwenye eneo lake ili wanafunzi wote watakaochaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari mwezi Januari mwakani wapate nafasi kwenye shule watakazopangiwa.
Jenerali Ibuge alisema,Serikali imetoa fedha nyingi za miradi kwa Halmashauri hiyo zikiwemo za utekelezaji wa miradi ya Covid-19 na lengo ni kuhakikisha miundombinu ya elimu ina kuwa bora na wanafunzi wanapata fursa ya kusoma na kufanya vizuri kwenye masomo.
Katika ziara hiyo ambayo alifuatana na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, alitembelea shule ya sekondari Nanungu,Mtakanini,Msindo, Nasuli na Narwi ambazo ujenzi wake uko katika hatua mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa, ameishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta ya elimu na afya ambayo itaongeza morali ya wanafunzi kusoma kwa bidii.
Hata hivyo alisema, changamoto kubwa ni kuchelewa kwa ujenzi wa miradi hiyo kutokana na upatikanaji wa vifaa kutoka kwa wafanya biashara waliopandisha bei ya vifaa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya hiyo Dkt Julius Ningu alisema,watafanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa mkoa na kuhaidi ujenzi wa vyumba vya madarasa vinavyojengwa vitakamilika kwa muda uliopangwa.
Mkuu wa shule ya sekondari Mtakanini Michael Kabogo alisema, wamepokea jumla ya Sh.milioni 40 kwa ajili ya kujenga vyumba viwili vya madarasa na hadi sasa fedha zilizotumika ni Sh. 12,937,700 na salio Sh.27,062,300.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.