MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewaapisha Wakuu wa Wilaya wapya, nakutoa maelekezo katika utendaji kazi wao.
Hafla ya kuwaapisha Wakuu wa Wilaya imefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali.
RC Ibuge amewaagiza Wakuu wa Wilaya wahakikishe wanasimamia wananchi kushiriki katika masuala ya Ulinzi na Usalama katika maeneo yao, kwa sababu hakuna maendeleo bila kuwa Ulinzi na Usalama.
“kasimamieni maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hakikisheni Miradi yote inayotekelezwa katika maeneo yenu, inakuwa yenye tija na kukamilika kwa wakati”. alisisitiza RC Ibuge.
Maagizo mengine aliyoyatoa Mkuu wa Mkoa kwa Wakuu wa Wilaya ni kuhakikisha thamani ya fedha katika Miradi inaonekana, kuhakikisha uwepo wa matumizi sahihi ya miradi iliwekezwa na Serikali na kuondoa na vikwazo katika ufanyaji biashara na kuhakikisha huduma zinapatikana kwa wakati na haraka.
RC Ibuge pia amewaagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia uwezeshaji wa Makundi maalum, ambayo ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa kuhakikisha asilimia 10 ya fedha ya mapato ya ndani, inatengwa kwa ajili ya kundi hilo.
Mkuu wa Mkoa amewataka Wakuu wa Wilaya katika maeneo yao wakahamasishe wananchi kujiunga na Bima ya Afya iliyoboreshwa, na kuhakikisha Fedha inayotakiwa kununuliwa madawa inawekwa benki.
Amesisitiza kuhakikisha Mazao ya kimkakati Soya, Ufuta, Mbaazi, Choroko na Korosho Kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani, ili wakulima watimize ndoto zao, Pamoja na kusimamia utekelezaji wa miradi inayotekelezwa na Taasisi za Umma zilizopo katika Halmashauri.
Ibuge amewaagiza Wakuu wa Wilaya kutatua kero za wananchi, na kusimamia ukusanyaji wa mapato na matumizi sahihi ya fedha za umma, kusimamia masuala ya elimu, na matumizi bora ya pembejeo za kilimo na elimu ya biashara na ujasiliamali kwa ajili ya kuboresha kipato kwa wananchi.
Kwa upande wake Mkuu Mpya wa Wilaya ya Nyasa Kanali Laban Thomas akizungumza baada ya kuapishwa, amehaidi kuwa Mtumishi, na kutokuwa mtawala na kujifunza kutoka kwa wananchi pamoja na kuchukua changamoto zao na kuzifanya kuwa fursa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mheshimiwa Julius Ningu ameahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili wanachi wa Namtumbo na anatarajia kujifunza mengi kutoka kwa wananchi wenyewe.
Mkoa wa Ruvuma una wilaya tano ambazo ni Songea, Tunduru, Namtumbo,Mbinga na Nyasa.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 22,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.