MKUU wa mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas,amewataka viongozi wa umma kwenda vijiji ili kutambua,kutatua shida na kuwaletea wananchi maendeleo,badala ya kutumia muda mwingi kukaa ofisini.Kanali Laban ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti,wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa wilaya ya Mbinga na Nyasa akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha wananchi kujiandaa na kushiriki kikamilifu zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23(kesho).
“watendaji wa umma acheni mambo ya kizamani ya kuvaa tai muda wote mkiwa ofisini,nendeni vijijini ili kuwasilikiza, kutatua kero na kuwaletea maendeleo wananchi mnaowaongoza”alisema.
Alisema, watumishi na viongozi wana wajibu wa kuitumikia jamii hasa katika maeneo ya vijijini ambako bado kuna changamoto nyingi na sio kukaa ofisini huku wamevaa tai na suti.
Aliongeza kuwa,viongozi wa aina hiyo hawana nafasi katika mkoa huo hivyo kwa kuwa hawatendi haki kwa wananchi na Rais Samia SuluhuHassan anayepambana usiku na mchana kutatua kero na kuboresha hali ya maisha kwa watu wake.
Laban alisema,wananchi wanahitaji sana kupata msaada na mchango wa viongozi wao kwa ajili ya kutatua kero na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na siyo kutanguliza maslahi binafsi.
Amewataka kushirikiana na wananchi katika maeneo yao,kubuni na kutafuta vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitachochea kukua kwa uchumi na kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Akiwa katika wilaya ya Nyasa,Mkuu wa mkoa amewakumbusha wananchi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanatunza chakula walichovuna katika msimu wa kilimo 2021/2022 kama tahadhari ya kukabiliana na uhaba wa chakula.
Kanali Laban alitumia fursa hiyo kuzuia matumizi ya mazao ya mahindi,muhogo na mpunga kutengeneza pombe kwa sababu kuna hatari ya kutokea kwa upungufu mkubwa wa chakula.
Aidha,amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Jimson Mhagama kuhakikisha anatekeleza na kukamilisha miradi yote ya maendeleo waliyoipanga katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Kanali Laban,amehaidi kupambana na watu wanaojihusisha na uvuvi haramu kwenye ziwa nyasa na wanaovua samaki wachanga ambao hawaruhusiwi kisheria kwa kuwa tabia hiyo inachangia sana kuadimika kwa samaki katika ziwa hilo.
Kuhusu sensa ya watu na makazi, Kanali Laban amewaomba wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kushiriki na kutoa ushirikiano kwa makarani watakaofika katika maeneo yao kwa ajili ya kupata taarifa zao na takwimu sahihi zitakazo wezesha Taifa kupanga mipango yake ya maendeleo.
Amewaasa kutoa taarifa zote muhimu na kwa makarani wa sensa,kuacha kuwaficha watu wenye ulemavu hasa watoto wadogo kwani kufanya hivyo ni kosa na hawatawatendea haki watoto wenye ulemavu.
Mkuu wa mkoa,amewashukuru wananchi na viongozi wa wilaya ya Nyasa kwa kumpa ushirikiano mkubwa wakati akiwa Mkuu wa wilaya hiyo kwa muda wa mwaka mmoja na miezi tisa na kuhaidi ataendelea kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Awali Mbunge wa Jimbo la Nyasa Stella Manyanya, ameiomba serikali kusimamia suala la uvuvi wa samaki wachanga wanaovuliwa katika ziwa hilo kwani tabia hiyo imesababisha samaki kupungua na umaskini mkubwa kwa wananchi wa Nyasa.
Kwa mujibu wa Manyanya,licha ya wilaya hiyo kuwa na utajiri mkubwa wa ziwa maarufu la Nyasa lenye samaki wa aina mbalimbali wakiwamo wa mapambo,hata hivyo ziwa hilo bado halijawanufaisha wananchi ambao wanakabiliwa na maisha duni.
Akizungumzia zoezi la sensa Manyanya alisema,wana Nyasa wana kiu kubwa ya maendeleo kwa hiyo ni muhimu kwao kushiriki kikamilifu zoezi ili kuisaidia serikali iweze kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.Alisema,serikali imeshatimiza wajibu wake kwa wananchi wa wilaya hiyo baada ya kukamilisha ujenzi wa Barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Mbambabay,kuimarisha Bandari ya Nyasa na kuleta meli za mizigo na abiria zinazofanya safari zake kati ya Nyasa mkoani Ruvuma na Kyela Mbeya.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.