SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi milioni 968 kujenga ofisi na nyumba tatu za watumishi katika shamba la miti Mpepo linalohudumiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Mpepo John Kimolo amesema mradi wa ujenzi unatekelezwa na Shirika la Nyumba NHC na kwamba jumla ya majengo manne yanajengwa ikiwemo Ofisi kuu ya shamba,nyumba ya Mhifadhi na nyumba mbili za watumishi.
Kimolo amesema serikali inatekeleza mradi huo kwa lengo la kuboresha mazingira bora ya kufanyia kazi na kuishi watumishi wa umma na kwamba mradi umefikia zaidi ya asilimia 95 ya utekelezaji.
“Lengo letu ni kuhamia Mpepo muda wowote,miundombinu ya mtandao wa intaneti na umeme vitakapokamilika kwa sababu shughuli za kiofisi zinahitaji mawasiliano ya mtandao’’,alisisitiza.
Hata hivyo amezitaja changamoto zinazoikabili ofisi hiyo kuwa ni ubovu wa barabara kutoka Nyoni hadi Mpepo inayopitika kwa shida hasa kipindi cha masika,ukosefu wa umeme na moto wa mara kwa mara hasa kipindi cha kiangazi unaosababishwa na wananchi wanapoandaa mashamba yao.
Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Ruvuma ukiwemo ujenzi wa ofisi za kisasa katika shamba la Mpepo.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amewaonya wananchi kuacha kuharibu mazingira kwa kuchoma moto na kuharibu mazingira kwenye vyanzo vya maji ambavyo amesema vinasababisha mabadiliko ya tabianchi.
Amewaagiza viongozi katika ngazi zote kusimamia na kuunda Kamati za Mazingira kwenye vijiji ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayechoma moto misitu na amewataka wananchi kuacha tabia ya kuandaa mashamba kwa kuchoma moto.
“Sisi ndiyo tunaochoma moto na kuharibu vyanzo vya maji,lakini sheria inasema kwenye vyanzo vyote vya maji ndani ya mita 60 hakuna shughuli yeyote ya kibinadamu inayotakiwa kufanyika,kuanzia sasa ni marufuku kulima au kufanya shughuli zozote kwenye vyanzo vya maji’’,alisisitiza.
Shamba la miti Mpepo ni miongoni mwa mashamba 24 ya miti yanayosimamiwa na kuhudumiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Novemba 19,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.