MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Julius Mtatiro,amewataka watumishi wa umma wilayani humo kufanya kazi kwa weledi,ufanisi ,kuzingatia taratibu na kanuni zilizopo kwa mujibu wa sheria ili kumrahisishia Rais Samia Suluhu Hassan baadhi ya majukumu na kazi ya kuwahudumi Watanzania.
Mtatiro ametoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na watumishi wa idara mbalimbali wa Halmashauri ya wilaya Tunduru katika cha kazi kilichofanyika katika ukumbi mdogo uliopo ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji mjini Tunduru.
Amewahimiza watumishi wa Halmashauri ya wilaya Tunduru wakiongozwa na wakuu wao wa idara, kuwa wabunifu sehemu za kazi wanapotekeleza majukumu yao,ikiwamo kuongeza kasi ya kukusanya mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato ili yaweze kuwahudumia wananchi.
“Mkuu wa idara anayesubiri fedha za sensa zifike na kuzigawa na baadaye anarudi ofisini badala ya kuumiza kichwa kutafuta vyanzo vya mapato huyo hafai kuwa kiongozi”alisema.
Kwa mujibu wa Mtatiro, mtu wa aina hiyo kimsingi ameshindwa kutimiza wajibu wake,kwa sababu sifa ya kiongozi lazima awe mfano kwa kutoa ushauri nini kifanyike kwenye idara yake.
“CMT nendeni mkafanye kazi ya kumsaidia Rais wetu kutekeleza majukumu yake,tukishindwa kukusanya na kusimamia mapato tunayokusanya ni dhahiri hatuna msaada wowote katika kumsaidia Mheshimiwa Rais Samia”alisema Mtatiro.
Alisema,mkuu wa idara atakayeshindwa kusimamia na kuibua vyanzo vipya vya mapato huyo hafai kuongoza idara na atakuwa hatendi haki kwa Rais wetu na wananchi katika wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine Mtatiro ameagiza vibanda vyote vinavyomilikiwa na Halmashauri vilivyopo eneo la stendi ya mabasi Tunduru mjini ambavyo hadi sasa havina wapangaji wapewe watu wenye mahitaji ambao watakuwa tayari kulipa pango na kodi mbalimbali za serikali.
Ametolea mfano baadhi ya vibanda vimepangishwa kwa Sh.30,000 lakini wapangaji hao wamewapangisha watu wengine kwa gharama kati ya Sh.150,000 hadi 200,000 kwa mwezi hivyo Halmashauri kukosa mapato makubwa badala yake watu wachache ndiyo wanaonufaika na uwekezaji huo.
Aidha,amewapongeza watumishi wa Halmashauri wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Chiza Marando kwa utendaji mzuri wa kazi na ushirikiano hali iliyosaidia shughuli nyingi za serikali kufanyika kwa wakati na ubora wa hali ya juu licha ya ukubwa wa eneo la wilaya hiyo.
Hata hivyo Mtatiro,amewaasa watumishi wote wa serikali katika wilaya hiyo kuacha kufanya kazi kwa mazoea,badala yake kuanza kubadilika katika utekelezaji na utendaji wa kazi zao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuipatia fedha wilaya hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema,katika kipindi cha mwaka mmoja Serikali imetoa fedha nyingi ambazo zimepelekwa kuboresha sekta ya afya,elimu na maeneo muhimu ya kipaumbele kwa ajili ya kuharakikisha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya na Taifa.
MWISHO
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.