Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma Mheshimiwa Ngollo Ng’waniduhu Malenya aliiagiza jumuiya ya watumia maji ya Likuyu na Mandela kuhakikisha wanaendelea kupanda miti na kuitunza ili kulinda mazingira ya chanzo hicho kisiharibiwe.
Akiongea na viongozi wa Jumuiya ya watumia maji wa Likuyuseka na Mandela pamoja na wataalamu kutoka Wakala wa Maji safi na usafi wa Mazingira vijijini(RUWASA) katika chanzo cha mto Namambigi na kusema kuwa chanzo cha mto Namambigi kinatakiwa kipandwe miti ya kutosha na kuitunza ili isife kwa kuwa chanzo hicho ndicho kinachotumika kusambaza maji katika kijiji cha Likuyuseka na Mandela.
Mkuu wa wilaya alikagua chanzo cha mto Namambigi na kukagua upandaji wa miti uliofanywa siku za nyuma na kubaini baadhi ya miti imekufa kwa kukosa uangalizi na kuiagiza jumuiya ya watumia maji kuhakikisha miti inayopandwa katika chanzo hicho inaangaliwa kwa karibu na kutunzwa.
Aidha Malenya alidai miti inayopandwa katika chanzo hicho inanunuliwa kwa shilingi 1000 kila mmoja ,hivyo kuiacha miti iliyopandwa bila uangalizi na kusababisha miti mingine kufa ni kupoteza fedha ,kupoteza muda lakini pia kupoteza mafuta yanayotumika kwenye magari .
Mjumbe wa bodi ya jumuiya ya watumia maji kijiji cha Likuyuseka na Mandela ,diwani wa kata ya Likuyu na makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo kassim Gunda alikiri miti mingine iliyopandwa kufa kwa kukosa uangalizi wa karibu kutoka kwenye uongozi wa jumuiya kwa kuwa miti hiyo ilipandwa nyakati za kiangazi na uangalizi wa mara kwa mara ulikosekana .
Meneja kutoka wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(RUWASA) David Mkondya alimwambia mkuu wa wilaya huyo kuwa usimamizi wa chanzo hicho ulikuwa unafanywa na jumuiya ya watumia maji na kutokana na hali hiyo wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini( RUWASA) itashirikiana na viongozi wa jumuiya katika kusimamia upandaji na utunzaji wa chanzo hicho
Wananchi wa kijiji cha Likuyuseka na Mandela kwa miaka mingi walikuwa wakilalamikia upatikanaji wa maji lakini kwa sasa serikali imejenga mradi mkubwa wa maji ya mtiririko na kuondoa kero ya upatikanaji wa maji na mto Namambigi maji yake hutumika kusambazwa katika vijiji hivyo viwili.
Mkuuwa wilaya huyo pamoja na wananchi na wataalamu walipanda miti 70 kwa siku hiyo wakati awamu mbili tofauti zilipanda miti 120 na miti 630 na kufanya jumla ya miti 820 iliyopandwa katika chanzo hicho huku miti 120 kati ya miti hiyo ilibainika imekufa kwa kukosa uangalizi wa karibu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.