MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma Pololet Mgema,amewataka wanafunzi wa kidato cha nne shule ya Sekondari Mkombozi,kutumia siku chache zilizobaki kusoma kwa bidii na kujikumbusha waliyofundishwa na walimu wao ili waweze kufanya vema katika mitihani ya Taifa inayotarajiwa kufanyika hivi karibuni nchini kote.
Mgema ametoa wito huo jana,wakati akizungumza na wanafunzi,walimu na wazazi kwenye mahafali ya pili ya kidato cha nne ambapo jumla ya wanafunzi 39 wanarajiwa kumaliza masomo yao siku chache zijazo..
Aidha,amewaonya kwenda kujiepusha na tabia ya ulevi,ndoa za mapema na ngono uzembe ambazo ni chanzo cha kupata magonjwa hatari ikiwamo ukimwi, na kukatisha ndoto zao.
Mgema ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo,ametoa onya kali kwa watu wazima kujiepusha kufanya mapenzi na wanafunzi ili kuepuka mikono ya sheria.
Badala yake,amewataka kuwa walinzi wa watoto hao ili wafanikiwe katika safari yao na hatimaye wawe viongozi bora watakao litumikia Taifa katika nyanja mbalimbali.
Amempongeza Mkurugenzi wa shule hiyo Franco Komba kutokana na jitihada zake za kuongeza miundombinu ya shule ambayo imewezesha kuwa na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia, hata hivyo ameshauri kutafuta walimu wazuri hasa wa masomo ya Sayansi ambao watakuwa chachu ya kuongezeka kwa taaluma katika shule hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Fidelis Komba,amewapongeza wahitimu hao kwa uvumilifu wao katika kipindi chote cha miaka minne,kwa kuwa walikutana na chagamoto mbalimbali wakati wa safari yao ya masomo.
Komba amewaasa vijana hao wanaotarajiwa kuhitimu kidato cha nne siku chache zijazo,kujiandaa vema na mitihani kwa kumshirikisha Mungu kwa kila jambo ikiwamo kufanya maombi ya mara kwa mara ili aweze kuwaongoza na kuwapa uwezo katika kujibu kwa usahihi maswali ya mitihani yao.
Hata hivyo amewakumbusha wanaporudi nyumbani,wakawe na maadili mema,kuwaheshimu wazazi na jamii inayowazunguka na kuheshimu sheria za nchi kama walivyokuwa wakiishi shuleni na siyo kwenda kuwa watu wa onyo na kukosa msaada wa jamii.
Katika hatua nyingine Komba,amewataka kuwa mfano bora na kwenda kuwasaidia wazazi wao kazi mbalimbali ili kuongeza kipato,badala ya kwenda kuwa mizigo isiyokuwa na faida kwa familia zao.
“wazazi msiwaache hawa watoto nyumbani mnapokwenda kwenye kazi za uzalishaji mali,nawaombeni sana muwe nao pamoja ili kuwafundisha kazi kama sehemu ya kujiandaa waweze kujitegemea watakapo kuwa watu wazima”alisema Mwalimu Komba.
Naye Mwalimu wa taaluma Jacob Kauzeni alisema,hayo ni mahafali ya pili ya kidato cha nne ambapo mwaka jana jumla ya wanafunzi 40 walihitimu masomo yao na kati ya hao wanafunzi sita daraja la1, wanafunzi kumi na sita walipata daraja la 2,wanafunzi kumi na nne walipata daraja la 3 na wanafunzi wa nne walipata daraja la nne na hakuna mwanafunzi aliyefeli.
Alisema, katika matokeo hayo wanafunzi wote walichaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano na baadhi yao walipata nafasi ya kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini.
Awali katika risala yao iliyosomwa na Jenifar Ndenga wahitimu hao,wamewapongeza walimu na mmiliki wa shule kuwapatia misingi imara itakayowawezesha kuwa na uwezo wa kujitegemea katika maisha yao.
Ndege alisema, hiyo ina miundombinu na mahitaji yote muhimu inayopaswa kuwepo kwa ajili ya wanafunzi wanaoishi bweni na wale wanaotoka nyumbani.Wameiomba Serikali kuisaidia shule hiyo kumaliza tatizo la maji,kwani sasa wanatumia maji ya kisima ambacho hakitoshelezi mahitaji ya wanafunzi waliopo na wakati mwingine wanalazimika kutumia vyanzo visivyo rasmi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.