WAKULIMA wa zao la korosho mkoani Ruvuma,wameuza jumla ya kilo milioni 1,248,620 kwa bei ya Sh.3,245 kwa kilo moja katika mnada wa kwanza uliofanyika katika Chama cha msingi cha Namitili kijiji cha Nakapanya kata ya Nakapanya.
Meneja Mkuu wa Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Tunduru(Tamcu)Marcelino Mrope alisema,katika msimu kilimo 2024/2025 malengo ni kukusanya na kuuza tani 28,000 ambazo ni zaidi ya tani 1,937 zilizokusanywa katika msimu wa kilimo 2023/2024.
Alisema,kati ya tani hizo wakulima wa mkoa wa Ruvuma wanatarajia kukusanya tani 27,950 na tani 50 zitakusanywa kutoka kwa wakulima wa mikoa mingine ikiwemo Njombe hasa wilaya ya Ludewa ambao wanahudumiwa na Chama kikuu cha Ushirika Tamcu.
Mrope alisema,katika msimu mauzo msimu wa 2024/2025 Tamcu itaendelea kutumia mfumo wa mauzo wa kimtandao(Online Trading System)unaosimamiwa na taasisi za ya Serikali ya soko la bidhaa Tanzania(TMX).
Aidha,katika msimu wa mauzo 2023/2024 jumla ya kilo 26,062,323 zilikusanywa na kuuzwa katika maghala makuu manane yaliyopewa kibali na bodi ya stakabadhi ghala ambapo uzalishaji uliongezeka ukilinganisha na msimu 2022/2023 ambapo kilo 15,317,972 zilikusanywa na kuuzwa ikiwa ni ongezeko la kilo 10,744,351 sawa na asilimia 70.1.
Alisema,katika msimu 2023/2024 korosho ziliuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghala kupitia minada na bei ilikuwa Sh.2,015 hadi Sh.1,345.
Alieleza kuwa,pamoja na mafanikio yaliyopatikana hata hivyo kulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya Amcos kutozingatia mwongozo unaotaka kupokea korosho zenye ubora katika maghala,kuwepo kwa maghala manane ambayo ni mengi badala ya matatu kama ilivyokuwa msimu 2021/2022 na sita ya msimu 2022/2023.
Kwa mujibu wa Mrope,kuwepo kwa maghala mengi kumesababisha watunza maghala kutozingatia ubora wakati wa kupokea korosho, hivyo kusababisha korosho kushuka ubora wake.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ya kusimamia sekta ya kilimo hapa nchini ambapo mkoa wa Ruvuma ni wanufaika wakubwa.
Ahmed alisema,katika msimu 2023/2024 changamoto kubwa ilikuwa kuchelewa kwa malipo ya wakulima,kukosekana kwa taarifa sahihi za uzalishaji(kanzi data)uzalishaji hafifu wa korosho,utoroshaji wa korosho,upotevu wa mazao na kukosekana kwa huduma za ugani kwa wakulima.
Amewataka wakulima kuendelea kuuza korosho zao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na kusisitiza malipo lazima yafanyike kupitia Chama kikuu cha Ushirika badala ya vyama vya msingi vya ushirika(Amcos).
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Simon Chacha alisema,wilaya ya Tunduru ni wazalishaji wakubwa wa zao la korosho katika mkoa wa Ruvuma na amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa zao la korosho.
Chacha amewataka watendaji wa vyama vya msingi vya ushirika(Amcos) na Chama kikuu(Tamcu)kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya Serikali yanayotaka fedha za wakulima kulipwa kwa wakati na kutumia mizani za Kidigitali kwenye kupima korosho na mazao mengine yanayouzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuepusha malalamiko kwa wakulima.
Mkurugenzi wa Bodi ya korosho Tanzania Francis Alfredy alisema,huo ni mnada wa kwanza wa korosho katika mkoa wa Ruvuma na minada kama hiyo imeshafanyika katika mkoa wa Mtwara na bei ilikuwa Sh.4,195 kwa kilo moja.
Alisema,mwenendo wa bei ya korosho katika soko la Dunia ilitegemewa kuwa kati ya Sh.3,000 hadi 3,600 kwa kilo moja,lakini jambo la kufurahisha bei ilipanda hadi kufikia Sh.4.000.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.