WAKULIMA wa kijiji cha Lukumbule Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,wameuza kilo 857,977.70 za ufuta zenye thamani ya Sh.bilioni 3,279,252,792.70 katika mnada wa kwanza uliofanyika katika viwanja vya Chama Kikuu cha msingi Nguvumali.
Katika mnada huo jumla ya makampuni 14 yalijitokeza kuomba kununua ufuta ambapo kampuni tatu za Yihayikerry Hysease,Mohamed Enterprises na Lenic Tanzania zilishinda baada ya kuomba kununua kwa bei ya wastani wa Sh.3,822 kwa kilo.
Akizungumza katika mnada huo Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro, amesisitiza suala la wakulima kuuza ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ulioonyesha mafanikio makubwa kwao,na kukataa kuuza kwa wafanya biashara wauni wanaopita mashambani ili kununua kwa bei ndogo.
Mtatiro,amewataka wanunuzi kuongeza bei ili kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa zao hilo mashambani,hatua ambayo itawasaidia kupata ufuta mwingi utakao zalishwa na wakulima kupitia vyama vyao vya msingi vya ushirika(Amcos).
Aidha amewahakikishia wakulima kuwa,Serikali haitachukua ela ya mkulima yoyote wa ufuta na mazao mengine yatakayozalishwa, na fedha zote zitakwenda kwa wakulima ili waweze kufaidika na nguvu zao kupitia shughuli zao za kilimo na uuzaji wa mazao yao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mtatiro alisema,badala yake serikali itaendelea kusimamia soko la mazao na tozo zilizopo kisheria ambazo haziwaumizi wakulima na kuwaonya wafanyabiashara wanaotaka kununua ufuta na mazao mengine ya wakulima kuzingatia sheria na kufuata utaratibu uliowekwa na serikali.
Pia,amewakumbusha wananchi kuhakikisha wanajiwekea akiba ya chakula kwa ajili ya familia zao na kuepuka tamaa ya kuuza chakula chote ili kupata fedha na umuhimu wa kuchangia chakula kwa watoto wao waliopo shuleni.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani humo Tamcu Ltd Mussa Manjaule,amewapongeza wakulima hao kutokana na uzalishaji mkubwa wa zao la ufuta katika msimu wa kilimo wa 2022/2023.
Manjaule alisema,wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wazalishaji wakubwa wa ufuta kila mwaka licha ya kukutana na changamoto mbalimbali na kuwataka wakulima wa maeneo mengine kwenda kujifunza kwa wenzao wa Lukumbule.
Awali Meneja Shughuli wa Tamcu Marcelino Mrope alisema,kuelekea msimu wa ufuta 2023/2024 Chama kikuu cha Ushirika Tunduru(Tamcu Ltd) kinarajia kukusanya ufuta kilo milioni 3,822,561 ikiwa ni zaidi ya kilo milioni1,273,746 kutoka kilo 2,548,815 ambazo zilizalishwa katika msimu 2022/2023.
Mrope alisema, katika msimu wa masoko wa mazao ya kilimo 2023/2024 Serikali imetoa mwongozo wa matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao ya ufuta,mbaazi, soya na korosho na Tamcu itaendelea kusimamia sheria na kutekeleza mwongozo huo mwa maslahi mapana kwa wakulima.
Aidha alieleza kuwa,wakulima wameendelea kufurahia mfumo huo kwa kuwa, una manufaa na faida kubwa kwao baada ya bei ya mazao yanayouzwa kupitia stakabadhi ghalani kupanda mwaka hadi mwaka ikilinganishwa na mfumo wa soko huria.
Baadhi ya wakulima wa kijiji hicho,wameishukuru serikali ya awamu ya sita kuendelea kusimamia soko la ufuta na mazao mengine kutokana na kupanda thamani na hivyo kufanikiwa kuwa na soko la uhakika na kupata bei nzuri.
Malaje Daud alisema kabla ya kuanza kwa mfumo huo miaka mitatu iliyopita ,bei ya mazao ilikuwa chini tofauti na sasa ambapo kupitia mfumo huo bei ya mazao yao imekuwa kubwa na hivyo wakulima wengi kuona kilimo kina manufaa makubwa.
Hata hivyo,ameiomba serikali iendelea kuwabana wanunuzi kwa kuongeze bei ya kununua mazao ili kuwahamasisha wakulima waendelee kuzalisha kwa wingi na minada hiyo ifanyike katika vijiji vyenye uzalishaji mkubwa.
Fenis Soka alisema,amefurahishwa na ongezeko la bei ya ufuta ikilinganishwa na mwaka jana,lakini ameiomba serikali kuhakikisha inawadhibiti wanyama wakali na waharibifu wanaoharibu na kula mazao mashambani.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.