Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema serikali inakwenda kutekeleza mradi mkubwa unaofadhiliwa na nchi ya India ambao unakwenda kumaliza kero ya maji katika Manispaa ya Songea.
Akizungumza ofisini kwake kuelekea maadhimisho ya wiki ya maji inayoanza Machi 16 hadi 22 mwaka huu,Mndeme amesema mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya India unagharimu zaidi ya Dola za Marekani milioni 45.3.
“Kinachoendelea hivi sasa kupitia Wizara yetu ya Maji,ni hatua za manunuzi ya wakandarasi wa kutekeleza mradi huo mkubwa ambao utahusisha ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji ambalo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita bilioni tano’’,alisema Mndeme.
Amesema mradi huo pia utahusisha upanuzi wa mtambo wa kusafisha maji na kutibu maji safi zaidi ya lita milioni 51.4 kwa siku,ujenzi wa matanki manne ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa lita milioni 18.2 na ulazaji wa mabomba yenye uwezo wa kusafirisha maji kilometa 190.3.
Mndeme amesema mradi huo utakapokamilika zaidi ya asilimia 95 ya wakazi wa Manispaa ya Songea watakuwa wanapata huduma ya maji safi na salama.
Amesema wananchi wa Manispaa ya Songea ambao hawajafikiwa na huduma ya maji,kupitia mradi huu mkubwa watapata maji na kuwezesha asilimia ya usambazaji maji kwenye manispaa hiyo kuongezeka toka asilimia 86.2 hadi 95 na kwamba lengo ni kufikia asilimia 100 ya kutoa maji katika miji ya Songea,Tunduru na Mbinga.
Hata hivyo amesema katika miji ya Mbinga na Tunduru serikali inatenga fedha kwenye bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya usambazaji wa huduma ya maji kwa wananchi.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga amesema ili miundombinu ya maji iwe endelevu, wananchi wanatakiwa kuilinda miundombinu na kuvitunza vyanzo vya maji kwa sababu serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi hiyo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 15,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.