Waandishi wa habari kutoka Klabu za Waandishi wa Habari Mkoa wa Ruvuma wamepatiwa mafunzo maalum ya ukaguzi yaliyolenga kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika kufuatilia matumizi ya rasilimali za umma na kuchochea uwajibikaji wa mamlaka kwa wananchi.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Songea Club chini ya uratibu wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), kupitia mpango wake wa kuimarisha ushirikiano na wadau wa habari katika shughuli za ukaguzi wa serikali.
Watoa mada wakuu katika mafunzo hayo walikuwa wataalamu wa mawasiliano kutoka NAOT akiwemo Bw. Nicolas Kilinga, Bi. Sakina Mfinanga na Bw. Focus Mauki, ambao waliwafundisha waandishi kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuandika taarifa zenye tija kwa jamii, pamoja na kushirikiana vyema na taasisi za umma katika kuhakikisha rasilimali zinatumika kwa ufanisi.
Katika mafunzo hayo, waandishi walipatiwa mbinu za kisasa za uandishi wa habari za ukaguzi, namna ya kuandaa na kuwasilisha ripoti zenye ushawishi wa kijamii, na umuhimu wa kutumia taaluma yao kama kiungo muhimu kati ya serikali na wananchi.
“Lengo ni kuwajengea waandishi uwezo wa kufuatilia kwa makini taarifa za ukaguzi na kushinikiza utekelezaji wa mapendekezo ya CAG kwa ajili ya maendeleo ya wananchi,” alisema Bw. Mauki.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Ruvuma, Amon Mtega, amepongeza juhudi hizo za NAOT na kuahidi kuwa waandishi wa Ruvuma wataendelea kushirikiana na serikali kwa karibu katika kuhakikisha uwazi na uwajibikaji vinapewa kipaumbele.
“Tunahakikisha maarifa haya tunayotumia kusaidia jamii kujua ukweli kuhusu matumizi ya fedha za umma,” alisema Mtega.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.