CHAMA Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Mbinga na Nyasa(MBIFACU) kimeanzisha shamba la miti la Kitelea mjini Mbinga lenye ukubwa wa hekari 39 lililopo kando kando ya barabara iendayo Mbambabay wilayani Nyasa.
Kaimu Meneja wa MBIFACU Henrick Ndimbo amesema chama hicho kimeanzisha shamba hilo kwa lengo la kujiongezea mapato na kuimarisha ushirika kutokana na maelekezo ya serikali ya awamu ya Tano yenye lengo la kufufua ushirika nchini.
Ndimbo amesema kupitia shamba hilo,katika msimu wa mwaka 2019/2020 MBIFACU imefanikiwa kuuza miti 118 yenye thamani ya shilingi 2,360,000/= na kwamba fedha hizo ziliingizwa kwenye mapato ya chama ili kuweza kusaidia uendeshaji wa shughuli mbalimbali za chama.
“Mpango mkakati wa mwaka 2020/2021 ni uvunaji wa miti kwa hekari 30 na uchanaji wa mbao ambazo zinatarajia kutuingizia kipato cha shilingi milioni 553,630,000/= baada ya kutoa gharama zote za uendeshaji,ikiwa ni moja ya juhudi za kuongeza mapato ya ndani ya chama ili kiweze kujitegemea’’,alisisitiza Ndimbo.
Ndimbo ametoa rai kwa Taasisi zote kushirikiana na MBIFACU katika kutekeleza na kusimamia mfumo wa ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima ambao unaweza kuwanufaisha wakulima,endapo mfumo wa ushirika utasimamiwa vizuri kupitia wataalam.
Amesisitiza kuwa ushirika utaongeza uzalishaji kwa kuongeza kipato cha wakulima moja kwa moja na kuongeza mapato ya Halmashauri ya serikali kwa ujumla.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa MBIFACU Winfred Lupembe amesema shamba la miti la Kitelea ni la miti ya zamani ambapo MBIFACU imeamua kuliboresha shamba hilo kwa kuvuna miti yote kwa matumizi ya mbao na kuni na kwamba baada ya kukamilisha kazi ya kuvuna,MBIFACU inatarajia kupanda miti upya kibiashara na kuingiza mapato makubwa zaidi.
Lupembe amesisitiza kuwa zoezi la uvunaji miti ya zamani na kupanda miti mipya linaendelea ambapo katika eneo hilo tayari imepandwa miti mipya 600 na kwamba shamba la miti linalomilikiwa na MBIFACU,ukitembea kwa mguu unaweza kutembea kwa saa mbili na nusu kuzunguka shamba lote.
Amesema miti yote ambayo ilipandwa katika shamba la miti la Kitelea ilishavunwa na kwamba miti iliyopo hivi sasa ni michipukizi ya miti zamani ambayo pia inavunwa kwa ajili ya mbao za kuendeleza mradi wa ukarabati wa hoteli ya MBICU kuwa katika viwango vya kimataifa.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Julai 11,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.