Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amekagua mradi wa chuo cha VETA Nyasa kinachojengwa katika kijiji cha Ruhekei Kata ya Kilosa Mbambabay kwa gharama ya shilingi bilioni 2.1.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa chuo hicho,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nyasa Jimson Mhagama amesema mradi huo utakuwa na majengo 15 na ulianza Aprili,2020 na unatarajia kukamilika Julai mwaka huu.
Amesema mradi huo unahusisha nyumba za watumishi,hosteli za wanachuo,bwalo la chakula, vyoo,madarasa na karakana na kwamba bati za kutosheleza majengo yote zimeshafika.
Kwa mujibu wa Mhagama, katika awamu ya kwanza ya ujenzi,serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni moja na kwamba hadi kukamilika kwa mradi huo utagharimu shilingi bilioni 2.1.
“Katika awamu ya kwanza ipo nyumba ya Mkuu wa chuo pekee yake,katika awamu nyingine zitajengwa nyumba za watumishi wengine,huu ni mradi mkubwa wa kwanza kutekelezwa kwa force account katika Halmashauri ya Nyasa’’,alisisitiza Mhagama.
Amesema mradi huo unatekelezwa na SUMA JKT ambapo hadi sasa utekelezaji wake unafanyika vizuri na kwamba ana matumaini makubwa kwamba utakamilika kwa wakati.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amemshukuru Rais Dkt John Magufuli kwa kutoa upendeleo maalum katika Mkoa wa Ruvuma,ambao sasa utakuwa na vyuo vya VETA vitatu ikiwemo cha Songea,Namtumbo na sasa chuo cha VETA Nyasa.
“Vyuo cha VETA vimekuwa vinajengwa makao makuu tu ya mikoa,lakini sisi wanaruvuma tumependelewa,wilaya tatu zinaenda kuwa na vyuo vya VETA,Songea na Namtumbo vyuo vinatoa mafunzo’’,alisisitiza Mndeme.
Amesema vyuo hivyo vitakwenda kuzalisha vijana ambao watakuwa na ujuzi mkubwa wa kuajiriwa na kujiajiri hivyo kuchangia kukuza uchumi wa Taifa kupitia fani mbalimbali zikiwemo ushonaji,ujenzi,ufundi magari, kompyuta,upishi na fani nyingine.
Katika Hatua nyingine Mkuu wa Mkoa amewashauri wanaosimamia ujenzi wa vyuo vya VETA nchini,kufanya michoro ya majengo kwa gharama nafuu,badala ya kutumia michoro inayotumika sasa yenye gharama kubwa na haiendani mazingira ya eneo la ujenzi.
IMEANDIKWA NA ALBANO MIDELO
AFISA HABARI WA MKOA WA RUVUMA
MEI 30,2020
MBAMBA BAY
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.