Jumla ya miradi 76 yenye thamani ya shilingi bilioni 96.8 inatarajiwa kutembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 katika Mkoa wa Ruvuma.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati anazungumza na wanahabari ofisini kwake mjini Songea kuhusu mbio maalum za Mwenge wa Uhuru ambao unaanza mbio zake mkoani Ruvuma Mei 9 na kukamilisha Mei16 mwaka huu.
Amesema miradi hiyo inajumuisha sekta muhimu kama afya, elimu, maji, barabara na huduma nyingine za kijamii na kwamba Kati ya miradi hiyo,miradi 17 itazinduliwa rasmi,miradi13 itawekewa jiwe la msingi na 33 itakaguliwa ili kuona utekelezaji wake.
Ameongeza kuwa miradi mingine 13 itahusisha ugawaji wa vifaa mbalimbali kwa wananchi. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na kwamba miradi hiyo inaonesha dhamira ya Serikali kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi.
Kwa mujibu wa ratiba ya mbio hizo, Mwenge wa Uhuru utakimbizwa kuanzia Mei 9 hadi 16, 2025 katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma kwa umbali wa jumla ya kilomita 1,378.90.
“Mwenge huo utaanza Halmashauri ya Madaba, kupita Songea, Mbinga, Nyasa, Mji wa Mbinga, Manispaa ya Songea, Namtumbo na kumalizia Tunduru’’,alisema Kanali Abbas.
Katika hotuba yake kwa wanahabari, Kanali Ahmed ameutaja ujumbe mkuu wa Mwenge wa Uhuru 2025 kuwa ni “Jitokeze kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa amani na utulivu”, ambao unalenga kuhamasisha wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao.
Mbali na kauli mbiu kuu hiyo,mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu pia zimejikita katika kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora, mapambano dhidi ya rushwa, VVU/UKIMWIna matumizi ya dawa za kulevya na malaria.
Kanali Ahmed amebainisha kuwa kampeni hizi zinaendelea kuwa silaha muhimu za kujenga taifa lenye afya, maadili na ustawi wa jamii.
Ametoa rai kwa wananchi wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kushuhudia hatua za utekelezaji wa miradi yao.
Amesisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru si tu ishara ya historia ya uhuru, bali pia chombo cha kuangaza maendeleo, ushirikiano na maandalizi ya uchaguzi wa amani mwaka 2025.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.