MWENGE wa Uhuru Kitaifa 2023 umeendelea na ziara yake katika wilaya ya Songea mkoani Ruvuma ambapo Aprili 19,2023 umekagua na kuridhia miradi yote katika Halmashauri ya Madaba yenye thamani ya shilingi milioni 859
Miongoni mwa miradi iliyoridhiwa na Mwenge wa Uhuru ni mradi wa ujenzi wa maji katika Kijiji cha Mbangamawe ambapo serikali kupitia RUWASA imetoa zaidi ya shilingi milioni 545 kutekeleza mradi huo.
Akitoa taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 ,Meneja wa RUWASA Wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles amesema mradi huo ukikamilika kwa asilimia 100 utawawezesha wakazi 2,800 kupata maji safi na salama ya bomba.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo,Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Ndugu Abdalla Shaib Kaim amewapongeza RUWASA kwa kuendelea kutekeleza miradi ya maji yenye viwango vinavyoendana na thamani ya fedha zilizotolewa na serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile kwa niaba ya wananchi amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha kujenga mradi wa maji katika Kijiji cha Mbangmawe ambacho hakijawahi kuwa na maji ya bomba tangu kuanzishwa kwake.Miradi mingine ambayo imetembelewa na Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Madaba ni mradi wa lishe katika zahanati ya Likarangilo na mradi wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika Kijiji cha Magingo.
Mwenge wa Uhuru pia ulikagua mradi wa utunzaji mazingira na kutembelea chanzo cha maji katika hifadhi ya misitu ya Wino inayosimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS),ambapo Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru amepongeza kazi kubwa inayofanywa na TFS kwenye utunzaji mazingira nchini.
Katika Halmashauri ya Madaba pia Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye mradi wa nyumba ya kulala wageni katika Kijiji cha Lilondo iliyojengwa na Mwananchi binafsi Ibrahimu Kilangwa kwa gharama ya shilingi milioni 126.
Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika Halmashauri ya Madaba pia ameweka jiwe la msingi katika kikundi cha Kwetu Madaba ambacho kimepewa mkopo na Halmashauri shilingi milioni 44 kufanya mradi wa kufyatua tofali za saruji.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.