Mwenge wa Uhuru ukiwa katika mbio zake mkoani Ruvuma, umeendelea kuangaza matumaini kwa wananchi kwa kupitia, kuzindua, na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.5 katika Wilaya ya Namtumbo pekee.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, amesema ameridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika wilaya hiyo, hususan miradi ya maji na elimu ambayo imeelezwa kuwa na ubora wa hali ya juu unaokidhi viwango vya kitaifa.
Katika hatua kubwa ya mapinduzi ya huduma ya maji safi na salama, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Msisima unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.1, ambao utahudumia wakazi 4,081 wa vijiji vya Msisima na Mnalawi.
Mhandisi David Mkondya, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Namtumbo, amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60, na unatarajiwa kuondoa kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi katika vijiji hivyo.
Mwenge wa Uhuru pia umefungua rasmi mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Mtakanini, unaotekelezwa kupitia programu ya BOOST kwa gharama ya shilingi milioni 107.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Namtumbo, Philemon Magesa, amesema ujenzi huo unakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wanafunzi darasani, hali inayoboresha mazingira ya ujifunzaji.
Katika kuimarisha huduma za kijamii na kiuchumi, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi kwenye kituo cha mafuta cha Anchr Oil Mtwara Pachani kilichopo Kata ya Luegu, kilichogharimu takribani shilingi milioni 160 hadi sasa.
Aidha, Mwenge umekagua vifaa vya kisasa vya meno vikiwemo dental chair na dental X-ray machine vilivyonunuliwa kwa shilingi milioni 18.94 kwa ajili ya Kituo cha Afya Lusewa, fedha zilizotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mkurugenzi Magesa amesema vifaa hivyo ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya ya kinywa na meno kwa wakazi wa eneo hilo.
Katika jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, Mwenge wa Uhuru umetoa mitungi 20 ya gesi safi yenye thamani ya shilingi milioni moja kwa wananchi wa Namtumbo. Magesa amesema Halmashauri inaendelea kutoa elimu kuhusu nishati safi ili kulinda afya na mazingira.
Akihitimisha ziara hiyo, Ismail Ussi ameipongeza Serikali ya Wilaya ya Namtumbo kwa kusimamia vizuri miradi ya kimkakati, hasa miradi ya maji na elimu, akieleza kuwa ni hatua madhubuti za kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amewezesha fedha nyingi kwa ajili ya miradi hiyo.
Amesisitiza kuwa miradi hiyo ni ya mfano na itakuwa na manufaa ya muda mrefu, hivyo wananchi wanapaswa kuithamini na kuitunza.
Mwenge wa Uhuru unaendelea na mbio zake katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma na unatarajiwa kukabidhiwa mkoani Mtwara Mei 17, 2025.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.