MBIO maalum za Mwenge wa uhuru mwaka 2021 zimekubali kuizindua na kuweka mawe ya msingi miradi yote nane katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.2
Kiongozi wa Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru mwaka huu Luteni Josephine Mwambashi ameikagua miradi yote kwa kushirikiana na wenzake na kuikubali miradi yote iliyopangwa kutembelewa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu.
Akisoma taarifa ya mradi wa katika kijiji cha Mkowela wilayani Tunduru,Mwakilishi wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Tunduru Emanuel Mfyoyi amesema mradi huo hadi kukamilika umegharimu zaidi ya shilingi milioni 163.
Amesema mradi huo umekamilika ukiwa na vituo vya umma saba vya kuchotea maji na vituo binafsi vinne na kwamba mradi huo una uwezo wa kuwahudumia wananchi 1,720 waliopo katika kijiji cha Mloweka.
Akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Muhwesi wilayani Tunduru kwa Kiongozi wa Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru,Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tunduru Beatrice Mahengu,amesema mradi huo ambao haujakamilika hadi sasa umegharimu shilingi milioni 80.
Amelitaja lengo kuu la mradi huo ni kuboresha huduma za afya kwa wananchi hasa mama na mtoto kwa kuwa
majengo ya zahanati iliyopo sasa ni machakavu hivyo yanaathiri huduma za afya.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Tunduru Patrick Haule akitoa taarifa ya ukarabati wa majengo ya Tunduru sekondari kwa kiongozi wa mbio maalum za Mwenge wa Uhuru,amesema serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 792 kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya shule hiyo.
Amesema mradi huo umekamilika na hivyo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa walimu na wanafunzi na kuboresha afya za wanafunzi baada ya kurekebisha mfumo wa maji safi na maji taka.
Miradi mingine ambayo imepitishwa na mwenge wa uhuru wilayani Tunduru ni mradi wa ugawaji wa vyandarua kwa akinamama wajawazito na watoto ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 94na mradi wa vifaa vya mahitaji maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu ya zaidi ya shilingi milioni nne.
Miradi mingine ni mradi wa TEHAMA katika chuo cha Maendeleo ya wananchi Nandembo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 100 na mradi wa ufugaji nyuki Nandembo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Septemba 2,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.