TAKUKURU waagizwa kuchunguza mradi wa sekondari ya Kawawa
MWENGE wa Uhuru 2023 umeridhia kuweka mawe ya msingi katika miradi mitano yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Chiriku Chilumba anautaja mradi wa kwanza kuwa ni wa ujenzi wa kliniki ya afya ya kinywa na meno katika hospitali ya wilaya ya Namtumbo ambao serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 320 kutekeleza mradi huo ambao unatarajia kukamilika Aprili 30 mwaka huu.
Mradi mwingine ambao Mwenge wa Uhuru umeridhia kuweka jiwe la msingi ni ujenzi wa daraja la Libango ambao hadi sasa serikali imetekeleza mradi huo katika awamu mbili kwa kutoa zaidi ya shilingi milioni 900.
Hata hivyo amesema katika utekelezaji wa awamu ya tatu,serikali inatarajia kutoa shilingi milioni 300 katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 ili kukamilisha mradi huo ambao utakuwa umetumia shilingi bilioni 1.2
Mwenge wa Uhuru pia umeridhia kuweka jiwe la msingi katika mradi binafsi wa mgahawa na kiwanda kidogo unatekelezwa mjini Namtumbo ambao unatarajia kugharimu shilingi milioni 120 ambapo hadi sasa kulingana na taarifa ya mmiliki wa mradi huo Romana Komba zimetumika shilingi milioni 80.
Komba amesema mradi huo unatarajia kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 20 na kwamba kiwanda kitakuwa na uwezo wa kutengeneza Mikate 1000 kwa siku na mgahawa una uwezo wa kutoa huduma kwa watu kati ya 50 hadi 100.
Mradi mwingine ambao Mwenge wa Uhuru umeridhia kuweka jiwe la msingi ni mradi wa ujenzi wa madarasa matatu katika shule ya sekondari ya Kawawa unaotekelezwa katika Kijiji cha Suluti ambapo serikali imetoa shilingi milioni 60 kutekeleza mradi huo.
Akizungumza baada ya kukagua mradi huo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Ndugu Abdalah Shaib Kaim amesema madarasa matatu yamejengwa katika ubora.
Hata hivyo amesema kuna dosari kubwa kwenye nyaraka za manunuzi ya vifaa ambazo zimebainika hazipo na kwamba meza na viti 115 zilizopo kwenye madarasa hayo ni mbovu na hazikuzingatia ubora unaotakiwa.
Kutokana na hali hiyo amemuagiza Mkuu wa TAKUKURU wilayani Namtumbo kufanya uchunguzi wa nyaraka za manunuzi na nyaraka za utoaji wa vifaa kutoka kwenye stoo.
“Afisa wa TAKUKURU ukibaini kuna upotevu wowote wa fedha za umma katika utekelezaji wa mradi huu sheria ichukue mkondo wake kwa mtu yeyote aliyehusika na upotevu huu’’,alisisitiza Shaib.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Aprili 18,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.