Mwenge wa Uhuru umetembelea miradi 11 yenye thamani ya shilingi bilioni 4.1 katika Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mheshimiwa Peres Magiri amesema Mwenge huo umekimbizwa umbali wa kilometa 284 na kwamba ukiwa kwenye mkesha wilayani humo wananchi walijitokeza kupima afya zao.
Amesema jumla ya watu 173 walijitokeza kupima Virusi vya UKIMWI(VVU) na hakuna hata mtu mmoja aliyepatikana na maambukizi ya VVU na wananchi pia walijitokeza kuchangia damu kwa hiari.
Moja ya miradi iliyozinduliwa na Mwenge wa Uhuru wilayani Tunduru ni mradi wa ujenzi wa jengo la kutolea huduma za dharura (EMD) katika hospitali ya wilaya ya Tunduru ambapo serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 369 kutekeleza mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo amesema mradi huo umekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi ambapo hadi sasa jumla ya wateja 1,003 wamepatiwa huduma kupitia mradi huo.
Mradi mwingine ambao umepitiwa na Mwenge wa Uhuru wilayani Tunduru ni ujenzi wa mradi wa maji safi katika Kijiji cha Tuwemacho ambapo serikali imetoa Zaidi ya shilingi bilioni moja kutekeleza mradi huo.
Meneja wa RUWASA wilayani Tunduru Mhandisi Maua Mgallah amesema mradi huo ukikamilika utawanufaisha wananchi wapatao 3,527 hivyo kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama.
Akizungumza baada ya kukagua mradi wa maji,Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Godfrey Mnzava ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo wa maji ambao amesema utapunguza changamoto ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata maji.
Miradi mingine iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru wilayani Tunduru ni mradi wa ugawaji wa vyandarua kwa akinamama wajawazito na Watoto ambao umewezesha wagonjwa wa malaria kupungua kutoka 99,469 mwaka 2021/2022 hadi wagonjwa 88,730 mwaka 2022/2023.
Mwenge wa Uhuru pia umetembelea mradi wa lishe,mradi wa ugawaji vifaa kwa makundi yenye mahitaji maalum na mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu ya familia mbili katika sekondari ya Kungu iliyojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 95.
Mradi mwingine ni wa kituo cha malezi ya vijana cha kilimo na mifugo la Kanisa la Upendo wa Kristo KIUMA ambapo mradi huo umegharimu Zaidi ya shilingi bilioni1.5,gharama zinazohusisha majengo, vitalu,nyumba,visima vya maji ya kumwagilia na mashine zake,bustani na mifugo
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.