Mwenge wa Uhuru umeendelea kung’ara katika Mkoa wa Ruvuma baada ya kuingia rasmi katika Manispaa ya Songea Mei 14, ambapo umepitia miradi nane ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.8, huku ukionesha kasi na dhamira ya kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi.
Kati ya miradi hiyo, Mwenge wa Uhuru umeweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa ujenzi wa maegesho ya magari makubwa katika eneo la Lilambo, mradi uliotengewa zaidi ya shilingi bilioni moja. Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashiri Muhoja, amesema hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 223 zimetumika, na kwamba mradi huo ni kichocheo muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa eneo hilo.
Katika hatua nyingine ya kuboresha huduma kwa jamii, Mwenge wa Uhuru umefungua duka la dawa katika hospitali ya Mjimwema. Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 68, fedha zilizotokana na mapato ya ndani, na utasaidia kupunguza usumbufu kwa wagonjwa kupata dawa muhimu kutoka MSD.
Aidha, Mwenge wa Uhuru umetembelea mradi wa utunzaji wa kisima cha asili kilichopo Kata ya Matogoro, kilichoboreshwa kwa zaidi ya shilingi milioni 23.9 na sasa kinahudumia kaya zaidi ya 500 kwa kutoa maji bure. Mzee Mohamed Said, mzaliwa wa mwaka 1936, alitoa eneo hilo bure kuunga mkono juhudi za serikali katika kutoa huduma ya maji safi na salama.
Katika kusukuma mbele ajira na maendeleo kwa vijana, Mwenge wa Uhuru pia umetembelea kikundi cha Super Group cha Kata ya Ruvuma kilichonufaika na mkopo wa shilingi milioni 15 kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Kikundi hicho ni mfano wa mafanikio ya mikopo isiyo na riba kwa vijana.
Kwa upande wa nishati mbadala, Mwenge wa Uhuru umekagua mradi wa matumizi ya gesi katika shule ya Good Shepherd Montessori. Mkuu wa shule hiyo, Joshua Sonsoge, amesema matumizi ya gesi yanapunguza gharama za kuni kutoka milioni 4 hadi milioni 3 kwa mwaka, hatua muhimu katika kulinda mazingira na kupunguza matumizi ya rasilimali za misitu.
Katika kuhakikisha watendaji wanakuwa na vifaa vya kazi, Mwenge wa Uhuru umegawa pikipiki 17 na vishikwambi 16 kwa watendaji wa Kata, kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 76, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa mbio hizo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismali Ali Ussi, amepongeza uongozi wa Manispaa ya Songea kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo. “Katika Manispaa ya Songea tumeona miradi iliyopangiliwa vizuri, utekelezaji wa viwango na ushirikishwaji wa wananchi. Hii ni mfano bora,” alisema.
Amehimiza wananchi kuitunza miundombinu hiyo na kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu mwezi Oktoba kwa amani na utulivu. Aidha, amesisitiza kuwa Mwenge wa Uhuru ni alama ya uzalendo na mshikamano wa kitaifa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwenge wa Uhuru unazunguka Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma tangu Mei 9 na unatarajiwa kukabidhiwa mkoani Mtwara Mei 17 mwaka huu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.