Mwenge wa uhuru umeendelea na mbio zake mkoani Ruvuma katika halmashauri ya Wilaya ya Songea na kuzindua jengo la matibabu ya wagonjwa wa dharula (EMD) katika hospitali ya rufaa ya misheni ya Mt. Joseph Peramiho.
Akitoa taarifa ya mradi wa jengo hilo, Mhandisi wa Hospitali hiyo, Greyson Nyirenda, amesema hospitali hiyo ilipata kiasi cha fedha Bilioni 1,317,870,928.58 kutoka kwa wafadhili ambao ni shirika la kidini kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.
Amebainisha kuwa mwaka 2022 idara hiyo ya wagonjwa wa dharula ilihudumia wagonjwa 49,263, mwaka 2023 wagonjwa 61,233 na baada ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo Novemba 2024 mpaka sasa wagonjwa 13,922 wameshahudumiwa.
Akizungumza katika hospitali hiyo kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa 2025, Bw. Isamail Ali Ussi, amesema kama kiongozi wa mbio za mwenge na wenzake wana imani kubwa na hospitali hiyo katika kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Naye Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe. Jenister Mhagama, amesema hospitali hiyo imekuwa ni kitovu cha huduma za afya kwa kuwa wananchi wa nyanda za kusini wanafika kupata huduma katika hospitali hiyo.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi za kidini na sekta binafsi ili kuhakikisha huduma za afya zinazidi kuwa bora na kuimarika katika nchi akisisitiza kuwa sekta hizo si washindani bali ni washiriki wa Serikali katika kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.