NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulika Menejimenti ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ramadhan Kailima amevitaja vipaumbele vyake vitatu vya kufuta hoja za ukaguzi.
Kailima amevitaja vipaumbele hivyo wakati anazungumza kwenye kikao kazi cha mawasilisho ya taarifa ya utekelezaji wa hoja za ukaguzi na maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za serikali za mitaa(LAAC).
Kikao kazi hicho kilichowashirikisha wakurugenzi wa Halmashauri zote nane za Mkoa wa Ruvuma,wakuu wa Idara na Menejimenti ya Mkoa kimefanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea Novemba 14 mwaka huu.
“Kipaumbele changu cha kwanza ni kufuta hoja za ukaguzi,kipaumbele changu cha pili ni kufuta hoja za ukaguzi na kipaumbele changu cha tatu ni kufuta hoja za ukaguzi,vipaumbele vyangu vyote vitatu ni kufuta hoja za ukaguzi’’,alisisitiza Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI.
Kailima amezitaja hoja za ukaguzi zikifutwa ujenzi wa miradi mbalimbali kama vile vyumba vya madarasa,barabara na vituo vya afya na miradi mingine,utafanyika kwa viwango na thamani ya fedha itaonekana.
“Sitakuwa na msamaha kwa mtendaji yeyote ambaye atakuwa anazalisha hoja kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake,ukizalisha hoja usitarajie kuhamishwa,biashara yako itaishia hapo hapo,utaondolewa kwenye nafasi uliopo’’,alisisitiza Naibu Katibu Mkuu.
Kulingana na Naibu Katibu Mkuu huyo,ukifuta hoja ya ukaguzi wa fedha kwenye benki,itasababisha fedha kupelekwa benki na mapato ya Halmashauri husika yataongezeka.
Ameongeza kuwa ukifuta hoja ya watumishi ambao hawajalipwa fedha zao za likizo,ni kwamba watumishi hao watalipwa fedha zao za likizo kwa wakati na kuboresha utendaji wao wa kazi.
Kwa mujibu wa Kailima,ukifuta hoja za malimbikizo ya watumishi na stahili zao mbalimbali,itawezesha watumishi hao kupata stahili zao kwa wakati na kupunguza manung’uniko kwa watumishi na kuongeza ufanisi wa kazi.
Hata hivyo amesema ukifuta hoja ya kununua bidhaa ambazo hazijapokelewa ina maana kuwa bidhaa hizo zitapolewa na kufuata taratibu za manunuzi hivyo hoja hazitakuwepo.
Amesisitiza kuwa hoja za ukaguzi zikifutwa zitawezesha viongozi wa kitaifa wakiwemo wabunge watakuwa wanaangalia thamani ya miradi iliyotekelezwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki akizungumza kwenye kikao kazi hicho amewaasa wakuu wa Idara kujibu hoja za ukaguzi kwa timu na kila mmoja kuwajibikaji kikamilifu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Mkoa wa Ruvuma
Novemba 14,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.