Naibu Waziri wa Maji MaryPrisca Mahundi amefanya ziara ya kikazi Wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kwa kukagua miradi ya maji ya mabilioni ya fedha.
Katika ziara hiyo Mahundi amekagua mradi wa maji wa Kipapa na Mhilo ambao umetekelezwa kwenye Kata za Kipapa na Langiro, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wenye thamani ya shilingi Milioni 647.4
Mradi huo umekamilika na umeanza kuhudumia wananchi kwa kutoa maji safi na salama.
Naibu Waziri wa Maji pia ametembelea na kukagua miradi mingine miwili ya maji ambayo ni mradi katika Kijiji cha Lifakara unaokadiriwa kugharimu Shilingi Milioni 651 na mradi unaojengwa Kata ya Bethlehemu ambao unatarajia kugharimu sh.Bilioni 1.4 hadi kukamilika kwake.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri wa maji pia amekagua miradi ya maji inayotekelezwa kwenye vijiji vya Amani Makolo, Mabuni, Luhagara na Litumbandyosi wilayani Mbinga.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo Naibu Waziri wa Maji ametoa mwezi mmoja kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Ruvuma(RUWASA) kuongeza vituo vya kuchotea maji kwenye kitongoji cha Kiosi, Kijiji cha Kipapa.
“RUWASA hakikisheni mnaanza utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji kwenye Kijiji cha Langiro Asili, Kata ya Langiro ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo’’,alisisitiza Mahundi.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshongwa ametoa rai kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji sanjari na miundominu ya maji iliyopo kwenye maeneo yao ili miradi hiyo iweze kudumu kwa muda mrefu na kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Aprili 12,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.