WATANZANIA wametakiwa kuwa na tabia ya kushirikiana na Serikali na kuiunga mkono katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji yenye mchango mkubwa katika kuchochea na kuharakisha maendeleo yao.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew ,wakati akizungumza na wananchi wa vijiji vya Misechela na Liwanga baada ya kuweka jiwe la msingi ujenzi wa mradi mkubwa wa maji unaotekelezwa na Serikali kwa gharama ya Sh.bilioni 3.02.
“Mambo makubwa yanayofanywa na Rais wetu Samia Suluhu Hassan,Mbunge wetu Idd Mpakate na Diwani wetu ni nzuri sana,kwa hiyo lazima tuwatie moyo na tuwaunge mkono,ili waendelee kufanya mambo makubwa zaidi”alisema Kundo.
Kundo alisema,Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan inawajali Watanzania ndiyo maana inawaletea na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo wilayani Tunduru na maeneo mengine hapa nchini ambayo imetoa fursa kwa wananchi kujikita kwenye shughuli zao za kiuchumi.
Alisema,kwa muda mkoa wa Ruvuma hususani wilaya ya Tunduru haikuwa na huduma ya maji ya uhakika,lakini katika kipindi kifupi Serikali sikivu ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta miradi zaidi ya 32 ya maji katika mkoa huo ikiwemo mradi wa maji Misechela.
Alisema,mradi wa Misechela utakapokamilika utamaliza kabisa changamoto ya huduma ya maji safi na salama na amewahakikishia wananchi kwamba mradi huo utakamilika kama Serikali ilivyopanga.
“Pia katika kupunguza changamoto ya maji katika jimbo la Tunduru kusini, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imechimba visima vya maji katika vijiji mbalimbali ikiwemo kijiji cha Mdingula na Azimio na kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali”alisema Kundo.
Kundo alisema,Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha mapenzi makubwa kwa wananchi wa Misechela kwa kutoa fedha nyingi ambazo zitatumika kutekeleza mradi huo ili kuwaondolea kero ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma ya maji.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Maua Mgallah alisema,mradi wa maji Misechela-Liwanga unaotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya Tunduru unategemewa kusambaza maji katika vijiji viwili vya Liwanga na Misechela na unatekelezwa kwa fedha za Serikali kupiti program ya malipo kwa matokeo(Pfor4).
Mgallah ametaja kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa tenki la ujazo wa lita laki tatu,ujenzi wa tenki la chini lenye uwezo wa kuhifadhi lita elfu sabini na tano na kujenga banio.
Kwa mujibu wa Mgalalah kazinyingine zilizopangwa kutekelezwa ni pamoja na uchimbaji mitaro na kulaza bomba, kujenga vituo vya kuchotea maji,nyumba ya mitambo,kufunga umeme jua na ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya watumia maji ngazi y jamii(CBWSO).
Pia alisema,wilaya ya Tunduru ina jumla ya vijiji 139 vinavyohudumiwa na Ruwasa kati ya hivyo vijiji 119 vimefikiwa na huduma ya maji na upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi ni wastani wa asilimia 70.20 ambayo ni sawa na watu 236,138 kati ya watu 336,380.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.