Baraza la Taifa la Hifadhi na usimamizi wa Mazingira NEMC limetoa siku 30 kwa wamiliki, waendeshaji wa Migodi na vituo vya kuuzia na kuhifadhia Makaa ya mawe kuhakikisha wanasajili miradi yao ili kupata vyeti vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na kuhakiki ndani ya siku 30 kuanzia Disemba 8, 2024.
Wito huo umetolewa kufuatia ukaguzi uliofanyika katika vitalu mbalimbali vya migodi na kubaini makosa yanayokiuka Sheria ya usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004.
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ofisi za Mkoa wa Ruvuma mara baada ya zoezi la ukaguzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria wa NEMC, Bw. Jamal Baruti ameorodhesha makosa yaliyobainishwa katika ukaguzi huo yakiwemo; Kutofanyika kwa Tathmini ya Athari za Mazingira (TAM), ukosefu wa mifumo ya usimamizi wa Mazingira, kutelekezwa kwa migodi pasipo kukarabati Mazingira, Uchafuzi wa vyanzo vya maji na hewa, kuongeza mawanda ya shughuli za migodi bila taarifa na idhini ya kisheria, kukosekana kwa taarifa za Upelembaji za kila mwaka na kukosekana kwa Mipango ya urejeshaji Mazingira.
Ukaguzi huo uliofanywa na timu ya wataalam kutoka NEMC kwa kushirikishana na wamiliki wa migodi umefanyika katika migodi 16 kati ya 18, maeneo ya biashara za makaa ya mawe 7 kati ya 15 na maeneo 2 ya utafiti kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 8, 2024 katika Wilaya za Madaba, Songea, Nyasa na Mbinga Mkoani Ruvuma.
Sambamba na hayo, timu hiyo ya ukaguzi imetoa elimu elekezi kwa wamiliki wa migodi ikiwemo kuweka miundombinu ya kudhibiti uchafuzi wa Mazingira, na ukarabati endelevu wa Mazingira,
Aidha Bw. Baruti amesisitiza kuwa Baraza litaendelea kutoa maelekezo na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara Kwa wamiliki wa migodi ili kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria na utekelezaji maagizo yaliyotolewa na kuto sita kuchukua hatua za kisheria kwa wadau wote watakaoshindwa kutekeleza maelekezo haya ikiwa ni pamoja na kupewa adhabu au kusimamisha shughuli zao ili kulinda Mazingira, afya ya jamii na kuhakikisha uwiano wa maendeleo ya kiuchumi, uhifadhi wa Mazingira na rasilimali za Taifa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.