Shirika lisilo la kiserikali la Nyasa Environment Restoration Initiative (NERI) la jijini Dar es Salaam limekabidhi zana za uvuvi na mizinga ya nyuki 20 kwa Kikundi cha Uvuvi cha Dagaa Safi katika kijiji cha Liweta, kata ya Mbaha, wilayani Nyasa. Pia, shirika hilo limekabidhi pikipiki moja kwa Afisa Uvuvi wa wilaya hiyo ili kuwezesha usafiri wake katika kulea kikundi hicho.
Akikabidhi vifaa hivyo katika ofisi za kikundi zilizopo katika mwalo wa Liweta, Mkurugenzi wa NERI, Bw. Daniel Nkondola, amewataka wanakikundi kutumia zana hizo kwa uvuvi endelevu na utunzaji wa mazingira. Vifaa hivyo ni boti nne, injini mbili za boti, nyavu za kuvulia dagaa, chanja za kisasa za kuanikia dagaa, mizinga ya nyuki, sare za kikundi, betri ya gari moja na pikipiki moja kwa Afisa Uvuvi.
Bw. Nkondola ameongeza kuwa ugawaji wa vifaa hivyo unalenga kuhamasisha uvuvi endelevu, uhifadhi wa rasilimali za uvuvi, na utunzaji wa mazingira. Pia, amesisitiza kuwa shirika hilo linatarajia vifaa hivyo vitawajengea wanakikundi uwezo wa kujiajiri, kuongeza kipato, na kupunguza umaskini kwa wakazi wa Wilaya ya Nyasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Bw. Khalid Khalif, amepongeza juhudi za NERI katika kukuza sekta ya uvuvi na kuhamasisha uvuvi wa kisasa. Aidha, ametoa wito kwa shirika hilo kuendeleza ushirikiano na jamii. Wanakikundi cha Dagaa Safi wameishukuru NERI kwa ufadhili huo, wakisema kuwa umewasaidia kutatua changamoto zao na kuboresha hali yao ya maisha.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.