SERIKALI imetangaza rasmi kuanza kununua mahindi kupitia wakala wa hifadhi ya Taifa(NFRA) Mei 15 kwa bei ya Sh 500 katika mikoa yote inayolima zao hilo,ikiwemo kwenye kituo cha NFRA Kanda ya Songea
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa kilimo Hussen Bashe, wakati akiongea na viongozi wadau wa kilimo na viongozi wa ngazi mbalimbali wa wilaya ya Tunduru katika kikao cha kazi ambacho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge.
Waziri Bashe amesema,Serikali imeamua kununua kwa bei ya 500 kutokana na wafanyabiashara kununua mahindi kwa Sh 250 ambayo hailingani na halisi ya uzalishaji, na hatua hiyo itasaidia sana kuwalinda wakulima ili kuwahi maandalizi ya msimu mpya wa kilimo 2021/2022.
Aidha, amewapongeza viongozi wa serikali ya wilaya ya Tunduru wakiongozwa na Mkuu wa wilaya Julius Mtatiro kwa kazi nzuri wanayofanya kusimamia suala la kilimo hususani kilimo cha zao maarufu la korosho ambalo ndilo linaloongoza kuipatia Serikali mapato makubwa ya fedha kigeni hapa nchini.
Amesema, lengo la wizara ya kilimo ni uzalishaji wa zao la korosho ni kuzalisha tani laki saba kwa mwaka,hata hivyo uzalishaji wa zao hilo unaendelea kuanguka kitakwimu ambapo katika wilaya hiyo inayosifika kwa uzalishaji hapa nchini unaendelea kushuka mwaka hadi mwaka.
Kwa mujibu wa Waziri Bashe,katika wilaya ya Tunduru uzalishaji umekuwa wa kusua sua kwani takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2016/2017 uzalishaji ulikuwa tani 15,310 mwaka 2017/2018 uzalishaji ulikuwa tani 20,000 mwaka 2018/2019 tani elfu 18, na mwaka 2020/2021 uzalishaji wa zao hilo ulishuka zaidi hadi kufikiwa tani elfu 14.
Amesema,ni lazima wadau wa kilimo wakiwemo wakulima wajiulize tatizo la kuongezeka kushuka kwa uzalishaji huo katika wilaya ya TunduruKwa mujibu wa Waziri Bashe,tatizo kubwa la kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo linatokana na watu waliopewa dhamana hasa wataalam wa kilimo kushindwa kuwafuatilia na kuwasimamia wakulima kwa kwa wakati kuwapa elimu ya kilimo bora jambo linalosababisha wakulima kuendelea na kilimo cha mazoea.
Hivyo amesema, Serikali ina wajibu kuhakikisha inawafuatilia wakulima kujua changamoto wanazokabiliana nazo na kuwapa elimu ya kilimo bora na chenye tija, badala ya kuwaacha wakiangaika na kuendelea kulima kwa mazoea.
Pia amesema, Serikali kupitia wizara ya kilimo imetafakari na kuamua kumuondolea mkulima mzigo wa pembejeo kwa kutoa pembejeo za ruzuku bure na mkazo mkubwa ni kupeleka dawa za maji badala ya dawa za unga na zitafikishwa kwa kila chama cha msingi cha Ushirika.
Amesema, matarajio katika wilaya hiyo ni kupata dawa za maji lita 130,000 na tayari lita 48,000,dawa aina ya Salphur kilo milioni 2.7 na ambazo zimeshafikishwa katika wilaya hiyo ni zaidi ya lita laki 9 ambapo wizara ya kilimo itahakikisha dawa zilizobaki zitawafikia wakulima.
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigadia Jenerali Wilbert Ibuge amemueleza Naibu Waziri kuwa, katika wilaya hiyo asilimia 85 ya ardhi yake inafaa kwa kilimo hata hivyo ni asilimia 15 tu ndiyo inayotumika kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Amesema, katika mkoa wa Ruvuma yenye watu takribani milioni 1.6 uzalishaji wa chakula kwa mwaka 2019/2020 ulikuwa tani 787.321 wakati mahitaji ilikuwa tani 469,172 hivyo kuwa na ziada ya chakula tani 318,149,mwaka 2021 uzalishaji ulikuwa tani 816,242 na hivyo kuwa na ziada ya tani 345,000.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro amesema,wilaya ya Tunduru imekuwa ikifanya vizuri katika uzalishaji wa mazao mbalimbali,hata hivyo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo Tembo wanaovamia mashamba na kuharibu mazao na ufugaji holela wa mifugo na kama changamoto hizo isipopatiwa majibu kwa haraka hali ya uzalishaji katika wilaya hiyo utashuka kwa kiwango kikubwa.
Mtatiro ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama amesema, changamoto nyingine ni kuwepo kwa Viuatilifu feki vinavyoingizwa sokoni na kuwauzia wakulima jambo linalokwamisha sana juhudi kubwa zinazofanywa na wakulima.
Amesema, katika wilaya hiyo asilimia 83 ya ardhi yake inafaa kwa kilimo cha mazao mbalimbali,hata hivyo bado wakulima wanahitaji maelekezo na msukumo wa wataalam ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija.
Imeandikwa na Muhidin Amri,Tunduru.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.