Na Albano Midelo
Ukitua wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, utajikuta katika mandhari ya kuvutia inayofanana na bustani ya asili iliyochorwa kwa mkono wa msanii wa kipekee.
Milima ya Umatengo imefunikwa na mistari ya kijani kibichi inayopanda na kushuka kwa ustadi wa ajabu na hapo ndipo unakutana na kile kinachoitwa Ngoro.
Sio tu kwamba Ngoro ni mfumo wa kilimo; ni urithi wa karne tatu, ni falsafa ya maisha, na ni ushahidi hai wa hekima ya jadi inayoshinda wakati.
Wakati ulimwengu unahangaika kutafuta njia za kilimo endelevu, Wamatengo wa Mbinga tayari walishaugundua ufumbuzi huo tangu karne ya 17.
“Ngoro si kilimo tu, ni njia ya kuishi. Ni urithi wa mababu zetu, uliotufundisha kulinda ardhi, kuheshimu mazingira na kulima kwa akili,” anasema Ngwatura Ndunguru, Mbunge Mstaafu wa Mbinga na mtaalamu mstaafu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kilimo Kilichobuniwa Katika Mapango
Ngoro ilizaliwa kutokana na hitaji la msingi: kuilinda ardhi dhidi ya mmomonyoko na kupunguza uharibifu wa rutuba.
Wakati jamii nyingine zilifanya kilimo cha kuhamahama, Wamatengo waliamua kutulia walikaa kwenye mapango na kuhitaji kilimo ambacho kingewezesha kuishi sehemu moja kwa muda mrefu bila kuhama.
Wakaanzisha mfumo wa Ingoro ambapo mashimo yanachimbwa kwa ustadi mkubwa milimani, nyasi zilizofyekwa hupangwa humo, na udongo wa chini hugeuzwa kuwa juu. Katika mzunguko wa miaka, majani hayo huchanganyika na udongo kuwa mboji yenye rutuba ya asili, na hivyo kurutubisha ardhi kila msimu.
“Kwa hakika, Ngoro ni kilimo cha kisayansi kilichozaliwa kwa majaribio ya asili. Hakuna mahali duniani kilimo kama hiki kimeandikwa au kutumika nje ya Mbinga,” anaongeza Ndunguru kwa msisitizo.
Kilimo Kinachovutia Hadi Kutazamwa Kama Utalii
Licha ya mafanikio yake katika uzalishaji wa chakula na uhifadhi wa mazingira, Ngoro pia imekuwa kivutio cha kipekee cha utalii.
Milima ya Mbinga imegeuka kuwa mandhari ya kushangaza: mistari ya mimea iliyoandaliwa kwa ustadi katika miteremko mikali ya milima, huonekana kama mapambo yaliyopambwa kwa mikono ya mbunifu.
“Wapo wageni wanaopita barabara ya Mbinga hulazimika kusimamisha magari yao ili kupiga picha, wengine hata video. Hawajawahi kuona kilimo kinachopendeza namna hii,” anaeleza Alex Ndunguru wa kijiji cha Ilela.
Ngoro si tu kivutio cha macho; ni somo la kimazingira, ni mfano wa namna jamii ya asili ilivyoweza kuoanisha kilimo na uhifadhi bila teknolojia ya kisasa, bila pembejeo za viwandani.
Ngoro Kama Suluhisho la Karne ya 21
Katika dunia inayokabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko wa udongo na ukame, Ngoro inasimama kama somo muhimu la kuchukuliwa kwa uzito.
Wakufunzi na watafiti kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakifika Mbinga kujifunza teknolojia hii ya kale ambayo inaonesha njia ya kwenda mbele kwa kilimo endelevu.
“Tangu tumeanza kutumia Ngoro, hatujawahi kuhama mashamba yetu. Tunazalisha chakula cha kutosha, tunatunza ardhi, na tunahifadhi mazingira yetu,” anasema mzee John Mbunda (80), mkazi wa Kilanga Juu.
Utafiti wa wataalam kama Bike (1938), Stenhouse (1994), Temu na Bisanda (1966) unaonesha wazi kuwa mfumo huu ulianzishwa mahsusi kuhifadhi rutuba katika miteremko ya milima ya Mbinga, jambo ambalo limewasaidia Wamatengo kuzalisha chakula bila kuharibu ardhi kwa zaidi ya karne tatu.
Ngoro ni Zaidi ya Kilimo – Ni Urithi wa Dunia
Ngoro si hadithi ya kale inayopaswa kufunikwa na vumbi la muda. Ni urithi hai wa Wamatengo ambao unapaswa kutambuliwa kimataifa kama mfano bora wa kilimo hai endelevu (agroecology).
Ni dhahiri kuwa jamii za asili kama Wamatengo walikuwa mbele ya wakati wao kwa kubuni mfumo wa kilimo ambao unaendana na mahitaji ya mazingira ya sasa.
Katika ulimwengu unaotafuta majibu ya jinsi ya kulima bila kuharibu mazingira, jibu linaweza kupatikana katika milima ya Mbinga kwenye Ngoro.
Ni wakati wa Tanzania na dunia nzima kuitazama Mbinga kwa jicho jipya: sio tu kama Wilaya ya kilimo, bali kama shule ya dunia ya kilimo cha asili kinachodumu.
Ngoro si tu mkombozi wa ardhi ya Umatengo; ni somo la dunia,Teknolojia ya ngolo ni Asilia ya Wamatengo Inayoshinda Mabadiliko ya Tabianchi, Ngoro ya Mbinga ni Urithi wa Kijani Unaovutia Dunia Nzima
Una maoni gani kuhusu kilimo cha asili cha ngolo? Tuma ujumbe wako kwa ajili ya kuendeleza mjadala huu muhimu kuhusu urithi wa kilimo cha asili wa Kitanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.