Matatizo ya mimba za utotoni hapa nchini yamekuwa yanaongezeka mwaka hadi mwaka hali ambayo inaathiri wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) inaitaja mikoa inayoongoza kwa kiwango kikubwa cha mimba za utotoni kuwa ni mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa asilimia 59,Tabora asilimia 58,Mara 55,Dodoma 51 na Lindi asilimia 48.
Mikoa mingine ni Mbeya asilimia 45,Singida asilimia 42,Rukwa asilimia 40,Ruvuma asilimia 39,Tanga asilimia,29,Arusha asilimia 27,Kilimanjaro asilimia 27, Kigoma asilimia 20,Dar es salaam asilimia 19 na Iringa asilimia nane.
Mkoa wa Dodoma umetajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa mimba na ndoa za utotoni ambapo asilimia 51 ya wasichana wenye miaka kati ya miaka 20 hadi 22 wameolewa kabla ya kufikia umri wa miaka 18 mkoani humo, ukilinganisha na asilimia 37 ya kitaifa kwa mujibu wa takwimu.
Kwa mujibu wa takwimu hizo kati ya watoto 100, watoto 51 wanaoolewa kabla ya kufikia miaka 18 katika mkoa wa Dodoma ambapo watoto wanaozaa wakiwa na umri mdogo ni asilimia 39.
Mkoa wa Dodoma umezindua kampeni ya kupambana na ndoa na mimba za utotoni ili kufikia malengo ya kumkomboa mtoto wa kike na kumuweka katika mazingira salama ya kumuwezesha kufikia ndoto zake badala ya kukatizwa na mimba za utotoni.
Mkakati unaotumiwa hivi sasa ni ule unaojulikana kama magauni manne ambayo ni mtoto wa kike kuwa ndani ya sare ya shule, gauni la pili ni la kuhitimu masomo,gauni la tatu ni la harusi na gauni la nne ni la kuvaa wakati wa ujauzito ambapo mtoto wa kike aatakuwa ametimiza ndoto zake.
Ukiacha Mkoa wa Dodoma,katika mwaka mmoja uliopita wa 2016/2017 Mkoa wa Tabora ulikuwa na jumla ya mimba za utotoni 800 hali iliyosababisha mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa mitatu nchini inayoongoza kwa mimba za utotoni.
Kukithiri kwa vitendo vya mimba za utotoni kumesababisha Rais Dk.John Magufuli kutoa agizo la wanafunzi wote katika shule za msingi na sekondari ambao watapata mimba hawataruhusiwa kuendelea na masomo.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.