Benki ya NMB imetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma vyenye thamani ya shilingi milioni kumi.
Akikabidhi vifaa katika hafla iliyofanyika katika hospitali hiyo mjini Namtumbo,Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Janeth Shango amevitaja vifaa hivyo kuwa ni vitanda vitano vya wagonjwa na godoro zake.
Vifaa vingine amevitaja kuwa ni vitanda viwili vya kisasa vitakavyotumika wakati wa kujifungua akinamama na mashuka 25 kwa ajili ya vitanda hivyo.
“Kwa miaka kadhaa sasa NMB imekuwa ikisaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi kwa kujikita zaidi kwenye miradi ya elimu kwa kutoa madawati na vifaa vya kuezekea na kwenye afya kwa kutoa vitanda na magodoro yake’’,alisema.
Amesisitiza kuwa kupitia jamii,NMB inatambua kuwa wanapatikana wateja wake wengi,kwa hiyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wa Benki hiyo ambayo imezifikia wilaya zote nchini kwa asilimia 100.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo ,Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Sophia Kizigo ameishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo ambao amesema umeongeza vitanda katika hospitali hiyo ambayo imeanza kulaza wagonjwa na kwamba kabla ya msaada huo ilikuwa na vitanda kumi tu.
“Tuliamua kuanzia mwaka jana kuanza kulaza wagonjwa,hivyo tulianza na vitanda kumi,leo NMB wametuletea vifaa vya milioni kumi kwa ajili ya kusaidia hospitali yetu,tunawashukuru sana’’,alisisitiza Kizigo.
Hata hivyo amesema NMB katika wilaya ya Namtumbo imekuwa karibu na shule kwa kutoa madawati na vifaa vya ujenzi na imetoa mikopo kwa ajili ya wakulima wa tumbaku.
Mary Ponera Mkazi wa Namtumbo ameishukuru NMB kwa msaada wa vitanda ambavyo amesema ni muhimu kwa wajawazito wakati wanafika kujifungua katika hospitali hiyo.
Benki ya NMB katika nchi nzima ina matawi 225,mashine za kutolea fedha ATM zaidi ya 800,wakala zaidi ya 6,000 na idadi ya wateja zaidi ya milioni tatu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Machi 10,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.