BENKI ya NMB imetoa msaada wa samani 70 kwa shule ya sekondari Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma zenye thamani ya shilingi milioni tano
Akizungumza katika hafla ya kutoa samani hizo iliyofanyika mjini Madaba Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Daniel Zake amesema Benki hiyo imetoa msaada huo Ikiwa ni sehemu ya kurudisha sehemu ya faida kwenye jamii.
Zake amezitaja samani zilizotolewa na NMB kuwa katika sekondari hiyo kuwa ni viti 50,meza 10 na makabati 10 na kwamba vifaa hivyo vitasaidia kuchangia ufaulu wa wanafunzi katika shule hiyo.
“Ni kawaida ya NMB kurudisha sehemu ya faida wanayoipata kwa jamii kwa kusaidia mambo mbalimbali yanayoizunguka jamii na leo tumeamua kutoa msaada huo katika sekta ya elimu na kupitia msaada wa vifaa hivi’’,alisema Zake.
Hata hivyo Kaimu Meneja huyo wa NMB Kanda ya Kusini ametoa rai kwa wanafunzi wa sekondari hiyo kuhakikisha elimu wanayoipata iweze kuwasaidia kujiajiri na kuweza kutengeneza ajira kwa watu wengine badala ya kutegemea kuajiriwa.
Akizungumza katika hafla hiyo mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema ameishukuru Benki ya NMB kwa msada huo ambao amesema imekuwa ni kawaida na utaratibu waliouweka wa kurudisha faida kwa jamii.
Mgema amewataka wanafunzi wa shule hiyo kutimiza wajibu wao wa kusoma kwa sababu serikali imejitahidi kujenga miundombinu ili wanafunzi waweze kupata elimu bora katika mazingira rafiki yanayovutia wanafunzi.
Nao baadhi ya wanafunzi wa sekondari wameishukuru benki ya NMB kwa kuwaletea vifaa hivyo na wameahidi kupitia vifaa hivyo wana uhakika wa kufanya vizuri katika masomo yao.
NMB ni miongoni mwa Benki zinazoongoza kwa wigo wa huduma za kibenki hapa nchini,ikiwa na matawi 228,mawakala zaidi ya 6,800,mashine za ATM zaidi ya 800,ikiwa na huduma za kibenki kwa njia ya mtandao,kituo cha huduma kwa wateja na vituo vya biashara.
Imeandikwa na Albano Midelo
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.