Benki ya NMB Tawi la Songea mkoani Ruvuma imezindua rasmi tisheti 500 zilizogharimu shilingi milioni tano kwa ajili ya Tamasha la Majimaji Selebuka spesho.
Tisheti hizo zitatumika kwa wanafunzi watakaoshiriki midaharo itakayofanyika kwenye tamasha hilo la Majimaji Selebuka ambalo litafanyika kwa siku saba katika uwanja wa Majimaji mjini Songea .
Akizungumzia Tamasha hilo Meneja wa NMB kanda ya kusini Janeth Shango amesema Tamasha hilo limelenga kuendeleza Utalii wa Mkoa wa Ruvumu,ujasiriamali na kukuza Michezo kwa wanafunzi na kwa watu wazima.
‘’ NMB tukiwa jirani ya jamii na kama wadau wa wajasiriamali, tumeona ni vema kushiriki katika tamasha hili ili tuweze kushirikiana na kusaidia kufanya tamasha hili liweze kuwa zuri zaidi mwaka huu’’,alisisitiza.
Shango amesema Benki ya NMB watakuwepo katika viwanja vya majimaji kwa wiki moja na watatoa huduma za kifedha na kutoa Elimu kwa wajasiriamali, na wanafunzi watafundishwa jinsi ya kujiwekea akiba, pamoja na mambo yote yanayohusiana na mikopo na ufunguzi wa akauntina namna ya kuendesha.
Hata hivyo Meneja wa NMB kanda ya kusini amesema watakuwa na wataalamu wa Kilimo na watatoa Elimu kwa wakulima jinsi gani wafanye wanapotaka kulima na kuvuna mazao kwa wingi.
Kwa upande wake Meneja wa NMB Tawi la Songea Daniel Zake amewashukuru wananchi kwa kuwa wateja wa Benki ya NMB ambapo katika tamasha hilo NMB watakuwa na masomo mbalimbali ya vikundi vidogovidogo,Benki jamii(VICOBA) na jinsi ya kujiwekea akiba kwa Fedha ndogo walizonazo ili kukuza kipato katika maisha yao.
‘’Tamasha la Maji maji Selebuka ni tamasha kubwa ambalo linakuwa na mambo mengi ya kujifunza hasa katika elimu ya Kifedha kwa upande wa mikopo na riba nafuu na kutumia mifumo ya kidijitali na namna gani unaweza kuwa nyumbani na kufanya miamala Mbalimbali na kuwahudumia waliombali kupitia simu ya mkononi’’,alisisitiza Zake.
Zake amesema Katika tamasha hilo itakuwa sehemu sahihi kupokea maoni kwa wateja wa NMB na jinsi gani wanaweze kufanya vizuri ka ili waweze kuhudumia wateja kwa kile wanachokitarajia wateja wa Mkoa wa Ruvuma kutoka Benki ya NMB.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari wa Mkoa wa Ruvuma
Agosti 11,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.