Kusini mwa Tanzania,mkoani Ruvuma kuna Wilaya ya Nyasa ambayo imesheheni hazina ya vivuti vya asili visivyochujuka.
Kutoka kwenye milima ya Livingstone inayoipamba Wilaya ya Nyasa hadi kwenye fukwe za ziwa Nyasa zenye mchanga laini wa mfinyanzi,Nyasa si tu wilaya, ni moyo wa vivutio adimu vilivyopo Tanzania.
Kwa muda mrefu, wilaya hii imebaki kama dhahabu iliyozikwa, lakini sasa inang’aa kwa matumaini mapya,ikiibuka kama kitovu kipya cha utalii wa kiikolojia, kiutamaduni, na kihistoria.
Mandhari ya Kipekee Inayochora Taswira ya Mbingu na Ardhi
Wilaya ya Nyasa ipo katika bonde la ufa la Afrika Mashariki, eneo ambalo lina umbo la kijiografia linalovutia kwa kupendeza na kutoa fursa ya mandhari isiyopatikana popote ndiyo maana Nyasa inaitwa peponi.
Bonde hilo linaonekana vizuri kutoka maeneo ya Buruma ukishuka kwenye kona za Ambrosi, ambapo maumbile yanakukaribisha kama vile yamepangwa kwa ustadi wa mchora ramani wa dunia.
Katika moyo wa wilaya hii, kuna Ziwa Nyasa,ziwa la tatu kwa ukubwa Afrika na la tisa duniani. Kwa kina cha kati ya mita 426 hadi 758, na maji meupe yenye kuvutia kama vioo vya asili, Ziwa hili ni mandhari ya ndoto kwa mpiga picha, mtafiti wa viumbe hai, na mwekezaji wa sekta ya utalii.
“Ni ziwa pekee duniani lenye aina zaidi ya 600 za samaki wa maji baridi, wakiwemo zaidi ya aina 400 wa samaki wa mapambo wanaopendwa barani Ulaya na Asia,” anasema Jonathan Ruanda, mtaalamu wa kuzamia samaki wa mapambo ambaye biashara yake imevuka mipaka hadi Marekani na Japani.
Visiwa na Fukwe zinazofaa kwa uwekezaji
Visiwa vya Mbambabay, Lundo,Puulu, Hongi na jiwe la Pomonda, kila kimoja kimebeba hadithi na historia yake.
Kisiwa cha Mbambabay kina mapango yanayotumiwa na wavuvi kujikinga na dhoruba.
Kisiwa cha Lundo kina historia ya wagonjwa wa ukoma waliotengwa na jamii, hali iliyosababisha kuibuka kwa imani ya kugandisha tope juu ya makaburi yao kwa matumaini ya kutibu ugonjwa huo.
Katika kisiwa cha Hongi,kuna taa ambayo iliwekwa kabla ya uhuru,ni mahali ambapo historia ya ukoloni, dini, na ujirani wa nchi jirani zinagusana kwa namna ya kipekee.
Liparamba: Pori la Akiba lenye Uhai wa Mwitu
Katika pori la akiba la Liparamba, wanyama kama tembo, simba, chui na mbwamwitu wanazunguka kwa uhuru.
Eneo hilo pia lina maporomoko ya Nakatuta ya mto Ruvuma, vivutio ambavyo ni urithi wa kimataifa wa ikolojia.
“Ni ushoroba hai wa wanyama wanaohama kutoka Tanzania hadi Msumbiji, na kurudi kulingana na majira,” anasema Afisa Maliasili Afrikanus Challe.
Zaidi ya hayo, ndege wanaohama kutoka Ulaya huja kutua mwambao mwa Ziwa Nyasa, wakiongeza mvuto wa kimataifa kwa watalii wanaopenda kuona viumbe wa ajabu.
Mambo Kale: Historia Inayosema kwa Mawe na Milango ya Nyumba
Afisa Maliasili Ali Limbega anabainisha kuwa historia ya dini na siasa inatiririka kwa kina wilayani Nyasa.
Katika kijiji cha Mbambabay, Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Nyerere na Hayati Oscar Kambona walilala mwaka 1956, wakipanga mikakati ya ukombozi wa Tanganyika.
Katika kijiji hicho hicho, Magavana wa Rodesia na Nyasaland walikutana mwaka 1959 kujadili mustakabali wa ukoloni. Majengo ya mbao yaliyowahifadhi bado yapo kama mashahidi wa historia.
Kanisa la Liuli lililojengwa kwa mawe mwaka 1939 na Padre Henrich Kunster linabeba historia ya Ukristo katika eneo hili.
Msikiti wa kwanza wa Kiislamu ulijengwa mwaka 1932 katika eneo la Ruhekei, ukianzia na ujio wa wafanyabiashara wa Uislamu waliokuja kupitia mito ya Lundo na Kimbande.
Ngoma, Imani na Utamaduni wa kuvuka Mpaka
Katika uwanja wa tamaduni, Wilaya ya Nyasa ni kisanduku cha hazina cha ngoma, vyakula na mila za kuvutia.
Ngoma za Lindeku, Mhambo, Chomanga, Kioda na Mganda huchezwa si tu kwa burudani, bali kwa kuenzi, kukosoa au kupongeza. Zilivuka mpaka hadi Msumbiji na Malawi,huu ni ushahidi kuwa utamaduni ni mto usiozuilika.
“Miongoni mwa vyakula vya asili vya Nyasa ni pamoja na ugali wa mihogo, mtama, ulezi na ngano.
Mboga zake za asili ni kama mlenda, mchicha libonongo na kisamvu. Vyakula vya kipekee kama kumbikumbi,likungu, chenene, viyenje na mbambwa hufanya sehemu ya urithi wa kitamaduni usio na mfano,” anasema Mbunge wa Nyasa Mhandisi Stella Manyanya.
Nyasa si Siri Tena, ni Fursa Iliyosubiriwa kwa Muda Mrefu
Wilaya ya Nyasa ni kitovu cha historia, uzuri wa asili, utajiri wa viumbe, na tamaduni hai ambazo bado hazijagusa macho ya dunia kwa kiwango stahiki.
Sasa ni wakati wa kuitangaza wilaya ya Nyasa ulimwenguni kote kama "Benki ya Utalii wa Tanzania."
Watanzania sasa wanashauriwa kusafiri, kuwekeza, kutangaza na kufurahia uzuri wa asili na fursa zilizopo katika Wilaya ya Nyasa.
Je, wewe ni msafiri, mwekezaji, mtafiti au mpigapicha picha? Nyasa inakusubiri, ndoto zako zitatimia.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.