Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amesema jitihada na mapambano yanahitajika ili kupunguza kiwango cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika mkoa huo.
Amesema hayo wakati akifanya uzinduzi rasmi wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo kitaifa itafanyika mkoani Ruvuma Disemba Mosi mwaka huu, ambapo uzinduzi huo umefanyika katika uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
"Kiwango cha maambukizi katika mkoa ni 4.9% kiwango hiki kimepungua ambapo tulikuwa katika wastani wa 5.6% kwa mwaka 2017, bado kiwango hiki ni cha juu, tunahitajika kuendeleza jitihada na mapambano ili kuweza kukipunguza kwa kiwango kinachotakiwa au kinachoelekezwa," alisema Kanali Ahmed.
Ameongeza kuwa maambukizi mapya yanatokana na vichocheo mbalimbali, hivyo amesisitiza kuendelea kudhibiti vichocheo hivyo na kutoa Elimu katika shughuli za kiuchumi zinavyoongezeka ili kupambana dhidi ya janga hilo.
Kupitia kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ambayo ni "Chagua Njia Sahihi, Tokomeza UKIMWI," Kanali Ahmed amewasisitiza wananchi kuendelea kuchagua njia sahihi kwa ajili ya kutokomeza UKIMWI.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Jumanne Issango, amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ya mwaka huu haiitaji ufafanuzi mkubwa kwa kuwa Elimu ya njia hizo zimekuwa zikitolewa katika majukwaa mbalimbali ili kuhimiza namna ya kutokomeza UKIMWI.
Ameongeza kuwa uchaguzi wa kauli mbiu hiyo ambao unaletwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kudhibiti UKIMWI ni hatua muafaka ambayo ikizingatiwa jamii itafika mahali pazuri.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dr. Catherine Joachim ameupongeza uongozi wa mkoa wa Ruvuma na wananchi wake wote kwa kupiga hatua katika mapambano dhidi ya VVU kwa kuwa katika mkoa wa Ruvuma kiwango chake kimepungua toka 5.6% kwa mwaka 2016/17 hadi 4.9% mwaka 2022.
Ameongeza kuwa takwimu zinaonyesha kuwa mkoa wa Ruvuma unaoongoza kwa upimaji wa VVU ambapo utafiti wa mwaka 2023 umeonyesha kuwa 82% ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma wanatambua hali zao za maambukizi na 97% ya watu wenye maambukizi wanatumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI.
Amesisitiza kuwa wao kama Wizara ya Afya inaukumbusha umma kuwa UKIMWI bado upo na ni janga la Taifa na bado unaendelea kusababisha vifo kwani hakuna chanjo wala tiba hivyo wananchi waendelee kuchagua njia sahihi ili kutokomeza UKIMWI.
Kiwango cha maambukizi ya virusi vya UKIMWI katika Mkoa wa Ruvuma kimeshuka kutoka 5.6% kwa mwaka 2016/17 hadi kufikia 4.9% mwaka 2022.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.